Mwakilishi wa kambi ya upinzani, Kemal Kilicdaroglu, amekua na jina maarufu nchini Uturuki kwa zaidi ya miongo miwili.
Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 74 wa chama cha Republican People's Party (CHP) amekuwa akijihusisha na siasa za Uturuki tangu 2002. Hata hivyo, katika harakati za kumng'oa Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan na chama chake tawala cha Haki na Maendeleo (AK Party), Kilicdaroglu anaonekana kutofua dafu kila wakati.
Kilicdaroglu, aliyekuwa akitambulika kama Karabulut kabla ya babake kubadili jina lao la ukoo , alizaliwa tarehe 17 Desemba 1948 katika mkoa wa Tunceli wa Uturuki akiwa mtoto wa nne kati ya saba.
Baada ya kupokea shahada yake ya kwanza ya uchumi katika Chuo Kikuu cha Gazi (hapo awali Chuo cha Uchumi na Sayansi ya Biashara cha Ankara) mnamo 1971, Kilicdaroglu alikua mtaalamu wa masuala ya fedha katika Wizara ya Fedha.
Baadaye alipandishwa cheo kuwa mhasibu na kupata mafunzo ya ziada nchini Ufaransa. Ndani ya wizara hiyo, baadaye aliteuliwa kuwa naibu mkurugenzi mkuu wa Idara ya Mapato.
Kabla ya kupanda kwenye jukwaa kuu la kisiasa, Kilicdaroglu alijulikana zaidi kama Rais wa Taasisi ya Bima ya Jamii (SSK). Alishikilia nafasi hii kuanzia mwaka 1992 hadi 1996.
Baadaye alichaguliwa tena kama rais wa SSK kutoka 1997 hadi 1999, lakini Kilicdaroglu hatimaye alistaafu kutoka SSK mwanzoni mwa 1999 huku macho yake yakitazama siasa.
Kujitosa kwenye siasa
Kilicdaroglu alijaribu kuingia kwenye orodha ya mgombea wa chama cha Uturuki cha Democratic Left Party (DSP) mwaka wa 1999, chini ya Waziri Mkuu wa zamani Bulent Ecevit, lakini licha ya kuitwa "nyota wa DSP" hakufanikiwa katika harakati hii.
Jitihada za aliyekuwa kiongozi wa wakati huo wa chama kingine cha CHP, Deniz Baykal, ndiyo zilimfungulia mlango mkubwa wa kisiasa Kilicdaroglu, na kumwalika kujiunga na chama chake. Baykal, pengine bila kujua, alianzisha kuinuka kwa mrithi wake.
Wakati akiwa Bungeni, Kilicdaroglu alianza kufungua njia ya kuongoza CHP kufuatia kujiuzulu kwa Baykal mwaka wa 2010.
Kama sehemu ya CHP, Kilicdaroglu alichaguliwa kuwa Mbunge katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2002 ambapo alihudumu kama mbunge wa moja ya majimbo ya kiuchaguzi ya Istanbul hadi mwaka 2015.
Kwanza, alikua naibu spika wa kundi la wabunge wa chama chake baada ya kuchaguliwa tena katika uchaguzi mkuu wa 2007.
Kisha mwaka wa 2009, aligombea Meya wa Istanbul kama mgombea wa CHP lakini akashindwa na mgombea wa Chama cha AK Kadir Topbas. Alipata asilimia 37 ya kura, huku Topbas akipata asilimia 44.71.
Mwaka mmoja baada ya kushindwa kwake katika mbio za Umeya, Kilicdaroglu aligombea uongozi wa CHP kufuatia kujiuzulu kwa Baykal kwa kashfa ya video. Video iliyochukuliwa kwa siri inadaiwa kufichua kuwa Baykal alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanachama mwandamizi ambaye aliwahi kuwa katibu wake.
Licha ya kukanusha tuhuma hizo na kutangaza kuwa kuna njama dhidi yake, Baykal aliachia ngazi na Kilicdaroglu aliishia kuungwa mkono na wenyeviti 77 wa mikoa kugombea nafasi yake. Katika kongamano la chama Mei 2010, alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa chama.
Akiwa kiongozi wa CHP, Kilicdaroglu pia alikua kiongozi mkuu wa upinzani kwani chama chake kilikuwa (na kinasalia kuwa) chama cha pili kwa ukubwa wa kisiasa katika Bunge Kuu la Kitaifa.
Jedwali la Sita
Kufuatia ushindi wake kama kiongozi wa CHP mwaka wa 2010, miezi michache tu baadaye, Kilicdaroglu alichukua msimamo katika kura ya maoni ya katiba iliyofanyika Septemba 12, 2010, ambapo alifanya kampeni ya kura ya "hapana" dhidi ya mageuzi ya katiba yaliyopendekezwa na Chama cha AK, na akashindwa.
Alijaribu hata kupinga mapendekezo hayo kisheria lakini Mahakama ya Kikatiba ilitoa uamuzi dhidi yake na mageuzi yakafanyika kwa asilimia 58 ya kura zilizounga mkono na asilimia 42 za kupinga.
Mwaka uliofuata, Kilicdaroglu alishiriki katika uchaguzi mkuu wa 2011 kama kiongozi wa CHP. Chama hicho kilipata asilimia 25.98 ya kura, ambazo ziliwaletea wabunge 135 waliochaguliwa, huku chama cha AK kilipata asilimia 49.83 ya kura na Nationalist Movement Party (MHP) kikipata asilimia 13.01.
Katika kipindi hiki, Kilicdaroglu aliwahi kuwa mbunge wa jimbo la uchaguzi la Izmir mnamo 2015.
Uchaguzi mkuu uliofuata wa Juni 2015 ulishuhudia Kilicdaroglu akipambana tena na Erdogan, lakini safari hii chama chake kilipata asilimia 24.95 ya kura, kikimaliza na wabunge watatu pungufu kuliko uchaguzi wa awali.
Katika uchaguzi wa 2018 ambapo, Muharrem Ince alikuwa mgombeaji urais katika uchaguzi mkuu, Kilicdaroglu alianzisha Muungano wa Kitaifa pamoja na viongozi mwenzake wa upinzani kutoka chama cha IYI, Meral Aksener, Temel Karamollaoglu wa Chama cha Saadet Party na Gultekin Uysal wa Chama cha Demokrat.
Muungano wa Kilicdaroglu ulipanuka mnamo Februari 2022: viongozi sita wa vyama vya upinzani, pamoja na wengine watatu, Ahmet Davutoglu wa chama cha Gelecek, Ali Babacan wa chama cha DEVA walijiunga rasmi. Muungano huu unajulikana kama "Jedwali la Sita".
Sasa kwa kuwa vyama vitano vya siasa vinaunga mkono ombi la Kilicdaroglu kuwa kiongozi wa Uturuki, je, atashinda uchaguzi wakati huu au Rais Erdogan atashinda tena? Kitendawili hiki kinasubiri majibu.