Uturuki itashiriki uchaguzi wa marudio Mei 28, huku Rais Recep Tayyip Erdogan akipata asilimia 49.5 ya kura - pungufu tu ya asilimia 50.1 ya kutangazwa mshindi - na mpinzani wake mkuu Kemal Kilicdaroglu akipata asilimia 44.89 pekee ya kura siku ya Jumapili.
Kwa wachambuzi wa masuala ya kisiasa, kufanyika kwa uchaguzi wa marudio nchini humo ni ushahidi wa kujitolea kwake kudumisha demokrasia.
"Ushiriki mkubwa wa Waturuki katika uchaguzi ulithibitisha utamaduni wenye mizizi ya demokrasia nchini Uturuki," Dk Ozden Zeynep Oktav, Profesa katika Idara ya Uhusiano wa Kimataifa katika Chuo Kikuu cha Istanbul Medeniyet aliiambia TRT World. Kwa jumla, zaidi ya vyama 30 vya kisiasa na wagombeaji wa ubunge huru 150 walichuana Jumapili.
Omer Celik, msemaji wa Chama cha AK alielezea umuhimu wa kufanya uchaguzi Uturuki, akibainisha "utajiri mkubwa wa nchi hii ni kwamba wananchi wanaamua ni nani ataitawala na kuongoza nchi hii."
Kwa jumla watu milioni 64.1 walijiandikisha kupiga kura, takriban wapiga kura milioni 5 wapya wakijiandikisha na karibu milioni 1.7 wakijiandikisha kupiga kura kutoka ng'ambo. Masanduku takriban192,000 ya kura yalitumika na upigaji kura ulifungwa mwendo wa saa kumi na moja jioni.
Kulingana na Balozi wa Marekani (mstaafu) Matthew Bryza, idadi kubwa ya wapiga kura wa Uturuki (89%) katika uchaguzi wa jana "ni maendeleo makubwa sana kwa demokrasia na idadi kama hiyo ya wapiga kura ni idadi ambayo Marekani ingetamani kupata katika chaguzi zake kwani yao inakadiriwa kuwa asilimia 65%.
"Idadi kubwa ya wapiga kura inaonyesha jinsi demokrasia ilivyo muhimu kwa raia wa Uturuki." Alisema Bryza, ambaye ni afisa wa zamani wa Ikulu ya Marekani.
Baadhi ya kura za maoni zilitabiri ushindi wa Kilicdaroglu huku Bryza akisisitiza jinsi zinavyoweza kuwa "sio sahihi", akilinganisha na uchaguzi wa Rais wa Marekani wa 2020 ambao "haukuwa sahihi" na uchaguzi wa 2016.
"Kwa hivyo sishangai kwamba kura za maoni kabla ya uchaguzi hazikuwa sahihi katika uchaguzi huu wa Uturuki ambao ulikuwa umemweka Kemal Kilicdaroglu mbele ya Rais Erdogan. Sidhani kama kuna jambo baya katika hilo - nadhani ni uamuzi tu wa wananchi. Upigaji wa kura za maoni ya umma katika nchi nyingi iikiwemo Marekani katika miaka ya hivi karibuni umekuwa si sahihi," alisema Bryza.
Hata hivyo, Oktav alisema "matokeo yalithibitisha kwamba kura za maoni za nje na habari za kumpinga Erdogan zilizotangazwa na vyombo vya habari vya kigeni hazikuonyesha ukweli. Aidha, kura hizo na habari ziliimarisha wazo kwamba Kiiıcdaroglu ni wakala wa Marekani. Hii ilisababisha kupungua kwa heshima ya Kilicdaroglu machoni pa wengi nchini Uturuki."
Katika kile ambacho kinaweza kuwa ni kura ya kwanza ya awamu ya pili chini ya mfumo mpya wa uchaguzi wa Uturuki ambao unaweza kufanyika Mei 28, wagombea wote wawili katika kinyang'anyiro cha urais, Rais Erdogan na Kilicdaroglu wameelezea matumaini yao, wakiamini kuwa wote wanaweza kushinda.
Bryza anaeleza kuwa "Ni ishara ya kukua kwa demokrasia ya Uturuki, kwamba wagombea wote wawili, Kilicdaroglu na Erdogan wanaamini wanaweza kushinda katika duru ya pili ya uchaguzi wa rais. Na pia nadhani ni nzuri, nzuri sana ikilinganishwa na Marekani. kwamba Rais aliyeketi Recep Tayyip Erdogan amesema mara kwa mara ataheshimu matokeo ya uchaguzi na tena sasa tunaona kwamba anakaribisha awamu ya pili."
"Hii ni kinyume kabisa na Marekani ambapo hata sasa, ghasia za Januari 6 huko Capitol Hill zilitilia shaka uhai wa taasisi za kidemokrasia za Marekani na ilikuwa ya aibu sana."
Bryza anasisitiza jinsi Rais Donald Trump hadi wiki iliyopita alikataa kusema kwamba atakubali matokeo yoyote ya uchaguzi wa rais wa 2024 alipoulizwa na mwandishi wa CNN Kaitlan Collins kwenye ukumbi wa jiji la CNN wiki iliyopita, akisisitiza kuwa atakubali matokeo, kama uchaguzi ni utakua wa haki tu."
"Anasema kwamba uchaguzi wa 2024 huenda usiwe wa haki na ikiwa atashindwa, itakuwa kwa sababu uchaguzi uliibiwa. Mfano uliowekwa na Rais Erdogan ni tofauti kabisa na mfano wa aibu wa Donald Trump," alisema Bryza.
Huku uchaguzi wa rais wa Uturuki ukifanyika mwaka wa 2023, Oktav anasisitiza umuhimu wa mwaka huu kwa waturuki wote kwa jumla kuhusiana na kuanzishwa kwa taifa hilo.
"Uchaguzi wa 2023 una maana kubwa kwa Waturuki kwani (mwaka) 2023 ni kumbukumbu ya miaka 100 ya Jamhuri ya Uturuki. Mbali na hilo, wengi waliamini kuwa Chama cha AK kingeshindwa katika uchaguzi huo kwa vile kimetawala kwa zaidi ya miaka 20 na kimekuwa kikikosolewa vikali. Kutokana na mfumuko mkubwa wa bei na matatizo ya kiuchumi.Cha kufurahisha ni kwamba kinyume chake kilitokea na chama cha AK kilipata kura nyingi bungeni." Alisema Oktav