Chama kikuu cha upinzani nchini Uturuki CHP chamchagua kiongozi mpya Ozgur Ozel

Chama kikuu cha upinzani nchini Uturuki CHP chamchagua kiongozi mpya Ozgur Ozel

Ozgur Ozel amechukua nafasi ya Kemal Kilicdaroglu na ataongoza CHP katika uchaguzi ujao wa mitaa mnamo Machi 31.
Kemal Kilicdaroglu ahudhuria Kongamano la 38 la Kawaida la Chama cha Republican People's Party (CHP) / Picha: AFP

Chama kikuu cha upinzani nchini Uturuki cha Republican People's Party [CHP] kimemchagua Ozgur Ozel kama kiongozi wake mpya, na kutamatisha muhula wa miaka 13 wa Kemal Kilicdaroglu, huku nchi ikijiandaa kwa uchaguzi muhimu wa mitaa utakaofanyika Machi 2024.

Ozel, 49, amekuwa akitumikia chama kama naibu mwenyekiti wa kikundi cha bunge cha chama hicho tangu 2015 na amekuwa mbunge tangu 2011.

Ozel alitangaza kugombea mnamo Septemba Baada ya Kilicdaroglu na CHP kushindwa na Rais Tayyip Erdogan na muungano wake wa kisiasa unaotawala mnamo Mei kwenye uchaguzi mkuu na wa urais.

Mnamo Jumamosi, Ozel alipokea kura 812 kati ya 1,366 zilizowezekana kupigwa katika mkutano wa chama uliochukua muda wa saa nyingi mjini Ankara ambao ulishuhudia raundi mbili.

"Hii ndio heshima kubwa maishani mwangu," Ozel alisema baada ya matokeo kutangazwa, akiongeza alimshukuru Kilicdaroglu kwa kazi yake kwenye chama hicho.

Kilicdaroglu alikosolewa kwa kukataa kujiuzulu kama kiongozi wa CHP baada ya kushindwa dhidi ya mrengo wa Rais Erdogan.

"Nilibeba urithi wa Kiongozi wetu mkuu Ataturk kwa heshima hadi leo," Kilicdaroglu alisema kwenye jukwaa la mtandao wa kijamii, X baada ya matokeo hayo na kumpongeza Ozel.

"Na hii leo, kufuatia uamuzi ambao wajumbe wetu walifanya, nasema kwaheri kwa wadhifa wa mwenyekiti."

TRT World