Cybercrime Africa

Na Mwandishi wetu

Mnamo tarehe 12 Agosti 2022, Benki Kuu na mdhibiti wa fedha nchini Afrika Kusini (SARB) ilikabiliwa na mashambulizi ya mtandaoni kutoka kwa wavamizi wasiojulikana.

Ingawa SARB ilidai miezi kadhaa baadaye kwamba udukuzi huo haukuathiri mifumo au uendeshaji wake, jambo linalotia hofu zaidi ni kufahamu kwamba Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI) ndio lilogundua na kuipa Benki hio taarifa ya udukuzi.

Ni wazi kuwa hadi wakati huo Benki hio haikufamu chochote kuhusu uvamizi huo.

Afrika Kusini haiko peke yake miongoni mwa nchi za Afrika ambazo Benki Kuu zake zinakumbwa udukuzi wa data. Miezi kadhaa kabla ya udukuzi wa SARB, Mei 2022, Benki Kuu ya Zambia nayo iliangukia kwenye kundi la wadukuzi waliotumia programu inayojulikana kama Hive.

Kwa mujibu wa chombo cha habari cha Bloomberg, Hive ilinyonya taarifa nyeti za kwa benki hiyo, na kutatiza baadhi ya mifumo ya kompyuta, ikiwemo mfumo wa unaoratibu ubadilishaji wa fedha.

Wadukuzi hao pia walidai kiasi cha fedha ambacho hakijawekwa bayana. Benki hio ilikataa kulipa.

Mwezi Novemba, Benki Kuu ya Gambia nayo ilipata mashambulizi mawili tofauti ya mtandao. Katika tukio la kwanza, wadukuzi walidai fidia ya dola milioni 2.5 ili wasivujishe taarifa za benki. Watumishi wa umma wa nchi hiyo walijikuta akaunti zao za benki zikifungwa.

Katika maeneo mengine barani, benki za biashara nchini Angola na Morocco pia zimeripoti mashambulizi ya mtandao kutoka kwa wadukuzi ambao wametishia kuweka hadharani taarifa nyeti.

Benki za kibiashara nchini Nigeria, kwa mfano, hupoteza dola milioni 30 kila mwaka kutokana na uhalifu wa mtandaoni.

Chanzo cha udukuzi huu kwenye taasisi za fedha za Afrika bado hakijajulikana, lakini Jarida la Afrika la Kiuchunguzi linakisia kuwa ongezeko hilo linatokana na vita kati ya Urusi na Ukraine (mwaka 2022) na kuwalazimisha wadukuzi wengi kuachana na Ulaya Mashariki ili kutafuta wahanga wengine.

Mnamo Aprili 2022, FBI ilidai kuwa Afrika Kusini na mataifa mengine ya Afrika yalikuwa sehemu ya kundi la nchi 135 ambazo miundombinu yao ilikuwa ikilengwa na wadukuzi wa Kirusi.

Wasiwasi juu ya usalama mtandaoni wa Afrika hauko kwenye mabenki tu.

Mnamo Machi 2022, idara ya kampuni inayojishughulisha na utoaji ripoti za mikopo ya Afrika Kusini, TransUnion, ilithibitisha kuwa kikundi cha wadukuzi chenye makazi yake nchini Brazili, N4ughtyssecTU, kilikuwa kimeiba taarifa nyingi zenye ujazo wa terabaiti 4 na kilikuwa kinadai fidia ya dola milioni 15.

Wadukuzi hao pia walitangaza kuwa walikuwa wakilenga makampuni mengine ya Kiafrika, ikiwa ni pamoja na Benki ya Absa.

Miezi michache baadaye, mnamo Juni, mfanyabiashara wa maduka makubwa wa kimataifa wa Afrika, ShopRite, ambayo ina takriban maduka 3,150 yanayohudumia wateja milioni 30, ilipata shambulio la wadukuzi kutoka kwa kundi la kigaidi la mtandaoni la RansomHouse.

Wadukuzi hao waliiba taarifa ya mteja sawa na gigabaiti 600, ikiwa ni pamoja na picha za vitambulisho vilivyotolewa na Serikali, na kutaka walipwe fidia.

Kati ya mwaka 2018 na 2022, taasisi za kifedha za Kiafrika zililengwa hususani na magaidi wa mtandaoni wa OPERA1ER wa Ufaransa.

Wakati huo, kundi hilo liliripotiwa kuiba dola milioni 11 kutoka kwa kampuni za Kiafrika, na uharibifu wake unakadiriwa kuwa na thamani ya dola milioni 30.

Kwa sasa, Afrika inapoteza dola bilioni 4 kila mwaka kutokana na uhalifu wa mtandaoni, na kugharimu bara hilo angalau 10% ya pato lake la ndani (GDP).

Gharama itaendelea kuongezeka huku uhalifu wa mtandaoni ukiongezeka barani Afrika. Kati ya robo tatu ya kwanza na ya pili ya mwaka 2022, kiongozi wa usalama wa mtandao Kaspersky aliripoti kwamba mashambulizi ya mtandaoni ya kuhadaa ili kupata taarifa binafsi— ambayo ndio aina maarufu zaidi ya uhalifu wa mtandaoni—iliongezeka kwa kiasi kikubwa, huku Kenya na Nigeria zikishuhudia ongezeko la 438% na 174% katika kipindi hicho.

Katika robo ya pili ya mwaka pekee, kati ya Aprili na Juni, Afrika ilirekodi zaidi ya mashambulizi ya hadaa milioni 10, ongezeko la 234% zaidi ya robo iliyopita. Kaspersky pia aliripoti kuwa 8.7% ya Waafrika walioko mtandaoni walipata mashambulizi ya hadaa mnamo 2022.

Ingawa njia ya hadaa inabakia kuwa aina ya uhalifu wa mtandaoni kote ulimwenguni na barani Afrika, uhalifu wa pesa za kidigitali (crypto) pia unaongezeka kwa kasi.

Kwa mwaka 2021 pekee, Wakenya walipoteza dola milioni 120 kwa uhalifu wa fedha za kidigitali huku Waafrika Kusini wakipoteza dola milioni 99, kulingana na ripoti ya Hali ya Utapeli Duniani.

Afrika Kusini pia imekuwa somo la kashfa mbili za utapeli uliovunja rekodi: kwanza, kampuni ya Mirror Trading International (MTI) iliwalaghai na kuwaibia maelfu ya watu takriban kiasi cha dola 589 milioni.

Baadaye, kampuni ya uwekezaji ya crypto ya Africrypt iliwalaghai wawekezaji takriban dola 3.6 bilioni za bitcoin (aina ya pesa za kidigitali). Dunia kote, zaidi ya dola bilioni 20 zilipotea kwa uhalifu huo mwaka wa 2022. Bado haijulikani kwa sasa kati ya hizo Afrika ilipoteza kiasi gani.

Mbali na ulaghai wa crypto, huduma ya kutuma pesa kwa kutumia simu ya mkononi, pia huchangia kuongezeka kwa viwango vya uhalifu wa mtandao barani Afrika.

Afrika inaongoza duniani katika soko la fedha kwa njia ya simu lenye thamani ya dola trilioni, ikiwa na asilimia 70 ya kiasi cha miamala ya sekta hiyo cha dola trilioni 1.04.

Sekta hii inakabiliwa na changamoto yake yenyewe ya uhalifu wa mtandaoni. Nchini Nigeria, kwa mfano, kampuni ya kutoa huduma za mawasiliano ya simu ya MTN, iliripoti wizi wa pesa wa dola 53 milioni miezi miwili tu baada ya kuzindua huduma za kutuma na kupokea pesa kwa simu nchini humo mnamo 2022.

Hivi majuzi zaidi, nchini Kenya, kampuni ya simu ya Safaricom ilitangaza kuwa ilikuwa mwathirika wa wizi mkubwa wa pesa kwa njia ya simu wenye thamani ya dola 4 milioni.

Habari njema ni kwamba Serikali za Kiafrika hazijapuuzia ongezeko la uhalifu mtandaoni. Hadi sasa, nchi 33 kati ya 54 za Afrika zikiwemo Nigeria, Afrika Kusini na Misri zimepitisha aina fulani ya sheria ya usalama wa mtandao.

Sio tu kwamba nchi zinatunga sheria za usalama wa mtandao, pia zinaunda sheria za ulinzi wa data zinazolazimisha makampuni kuweka kanuni muhimu za usalama wa mtandao.

Shirika la Polisi la Kimataifa (Interpol) linaripoti kuwa angalau 90% ya biashara za Kiafrika zinafanya kazi bila kanunuzi hizo za usalama wa mtandao.

Pia kuna mashirika kama Ciberobs na TradePass yanayoandaa mikutano ya usalama wa mtandao kama vile Cyberx Africa Summit nchini Kenya, na Cyber ​​Africa Forum nchini Côte d'Ivoire.

Makongamano haya, yanayohudhuriwa na maelfu ya watu duniani kote, yanahamasisha watumiaji na makampuni kuhusu umuhimu wa usalama wa mtandao. "Kujenga ufahamu ndio jambo kubwa tunalofanya kwa sasa. Watu wanahitaji kujua kuhusu hatari zilizopo na usalama mtandaoni," alisema Franck Kie, manager mkuu wa Ciberobs katika mahojiano na TechCabal mwaka jana.

"Nchi kama Morocco, Mauritius, Kenya, Togo, Afrika Kusini, na hata Côte d'Ivoire bila shaka zinaweka usalama wa mtandao kama vipaumbele vyao vya juu."

Kutokana na ongezeko la orodha ya sheria za usalama wa mtandao, mikutano na wataalam, ni wazi Afrika inaweza kukabiliana na vitisho vyake vinavyo ongezeka vya usalama wa mtandao.

TRT Afrika