Waziri wa Madini Tanzania Anthony Mavunde. Picha/TRT Afrika. 

Waziri wa Madini nchini Tanzania Anthoy Mavunde amesema Serikali haijakurupuka kufuta leseni za wamiliki waliobainika kuwa hawaendelezi maeneo yao na badala yake amesitisitiza kuwa, zoezi hilo linaendeshwa kwa kuzingatia sheria na taratibu za nchi.

Mavunde ameongeza kusema kuwa baadhi ya watu wanaoshutumu mitandaoni kwamba Waziri hajashauriwa vyema wanajidanganya na kwamba nia yake ni kuendelea kuzifuta leseni nyengine hadi pale wizara itakapowapata watu sahihi.

“Nimeanza kuona wanaandika katika mitandao kwamba Waziri hajashauriwa vizuri, nataka niwaambie wale wote ambao wanafikiri tumekurupuka, hatujakurupuka,” alifafanua Mavunde.

Waziri huyo amewaambia waandishi wa habari mkoani Dodoma kwamba wizara imebaini kuwepo kwa watu 6 wanaoshikilia maeneo yenye ukubwa wa hekari milioni 13 ambazo ni sawa na mikoa minne ya Kilimanjaro na hawaendelezi na kuonesha ni kwa kiasi gani watu wanatumia vibaya leseni.

Amewaonya pia wamiliki wa akaunti za uombaji na usimamizi wa leseni kwa njia ya mtandao, wenye matumizi mabaya ya kimfumo juu ya umiliki wa maeneo.

“Wamekuwa wakitumia fursa ya uwepo wa teknolojia rahisi ya uwasilishaji wa maombi ya leseni - yaani mfumo wa Online Mining Cadastre Portal vibaya kwa kuwasilisha maombi mengi bila ya kulipa ada stahiki na wengine kuwasilisha maombi bila ya nyaraka stahiki zinazotakiwa kuwasilishwa pamoja na maombi ya leseni,” amesema.

“Hii nchi ya kwetu sote, wajanja wachache wasijifanye wanajua sana kuliko watu wengine ambao ukiwagusa kidogo malalamiko mengi sana,” ameongeza.

Onyo hilo liliambatana na maelekezo kwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini la kufuta jumla ya maombi ya leseni 2,648 kwa wamiliki wa leseni hizo ambao hawajaendeleza maeneo yao, ili kupisha waombaji wengine kupata fursa ya kuyamiliki na kuyaendeleza.

Kwa miaka mingi sekta ya madini nchini Tanzania imekuwa ikilalamikiwa kuhusu kutonufaisha wazawa licha ya mchango wake kuongezeka kutoka asilimia 4.4 mwaka 2017, hadi asilimia 7.2 mwaka 2021. Na katika katika kipindi cha robo ya tatu ya mwaka 2022/2023 mchango wa sekta hiyo umefikia asilimia 9.6.

Takwimu hizi ni kwa mujibu wa Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa alipozitoa mwaka jana katika ufunguzi wa kongamano la wachimbaji madini na Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Madini Tanzania (FEMATA).

TRT Afrika