Zaidi wa wanawake wazee 30 nchini Kenya wameunda kikundi kinachojifunza mchezo wa karate kwa lengo la kujilinda na visa vya uhalifu. Picha/TRT Afrika. 

Job Samuel

TRT Afrika, Nairobi, Kenya

Kutana na kikundi cha wanawake wazee 20 wa kenya waliojifunza Karate kukabiliana na vitendo vya uwizi na ubakaji katika kijiji cha Korogocho, jijini Nairobi nchini kenya.

Korogocho ni mojawapo ya vitongoji duni vilivyo na idadi kubwa ya watu jijini Nairobi, ambapo ubakaji na wizi ulikuwa wa kawaida.

"Tulianzisha kikundi hiki mwaka 2007 tulipogundua kuwa wanawake wazee walilengwa sana na wabakaji na waizi," Beatrice Nyariara, Mwenyekiti wa kikundi cha Shosho Jikinge anasema.

Vitendo vya ubakaji vilikithiri katika eneo hilo, baada ya baadhi ya vijana katika eneo hilo kuamini kwamba, kufanya mapenzi na wanawake wazee kunaweza kutibu virusi vya Ukimwi, huku wengine wakiamini kuwa kunaweza kuwaondolea mikosi.

Kikundi cha wazee hao kina wanachama kuanzia miaka 60 hadi 94. Picha/TRT Afrika. 

Mdogo zaidi wa wanawake hawa wazee ana miaka 60 na yule mwenye umri mkubwa akiwa na umri wa miaka 94. Ujuzi wao wa ngumi na kurusha mateke wanasema umewafaa.

Msafiri mmoja kwa Jina ‘Jake’ aliyekuwa akitembelea eneo hilo alipata fursa ya kuelezwa masaibu yaliyowakumba wanawawake na wanaume wazee katika eneo hilo. Aliwahurumia na kuanza kuwapa mafunzo ya kuwalinda na kuwaelimisha jinsi ya kupambana na mwizi au mbakaji.

’’Alituambia tuunde kikundi. Baada ya siku kadhaa, alituletea mke wake. Mke wake alikua anakuwa na maarifa ya kupigana karate. Alitufunza kwa muda wa miezi sita. Wiki mbili za kwanza tulikua na maumivu makali, kwa sababu ya kufanya mazoezi. Miili yetu imezeeka. Karibu hata tuache kufanya mazoezi," amesema Beatrice Nyariara, mmoja wa waanzilishi.

Walibuni jina la kikundi hicho na kujiita, ‘Shosho’ Jikinge. ’Shosho’ni jina la kabila moja nchini Kenya, lenye maana, 'bibi' au 'mwanamke mzee.' Na hiyo ndio iliyokuwa maana halisi ya kikundi hivyo, ya kutaka wanawake hao kujilinda.

Wana gunia la ndondi wanalotitumia kufanyia mazoezi. Wamejifunza mahala pa kumpiga mhalifu na kisha kupiga mayowe wakiitisha usaidizi.

Wamejifunza kuwa huwa wanampiga mhalifu teke sehemu ya chini ya kiuno, katikati ya miguu, au kwenye pua ama utosini huku wakipiga mayowe ya kuomba msaada.

Kina mama hawa wanasema, tangu kuanza kujifunza karate, uhalifu umepungua kijijini hapo. Picha/TRT Afrika. 

Mafunzo hayo pia yanawaelekeza kina mama hao, iwapo wangetaka kufanikiwa kujinusuru, jinsi ya kuwashambulia washambuliaji kwa nguvu katika sehemu za mwili ambazo watawapa maumivu mno.

Maneno yao, wanayoyatumia pindi wanapovamiwa na vibaka ni kama, "Hapana! Wachana na mimi! Niachilie! Njooni mnisaide jamani!" Wanasema hivyo huku wakijaribu kukimbia kutoka eneo la uhalifu.

"Tunakuja kufanya mafunzo kwa masaa mawili kwa siku, mara nne au tano kwa wiki. Baada ya hapo kila mmoja wetu anaelekelea kutafuta chakula cha kila siku kusaidia familia yake. Iwapo kuna yeyote pale nje ambaye pia angependa kutusaidia kwa vyovyote vile, tutashukuru" anasema Grace Ngánga, mwanachama wa Shosho Jikinge.

Maarifa kuhusu mafunzo yanayoendelea kwa wanawake hawa yameenea kijijini kama moto msituni wakati wa kiangazi. Hii imewafanya washambuliaji wengi kuogopa na baada ya muda matukio ya ubakaji yanayowalenga wazee yamekua yakipungua.

’’Kikundi hiki kimetusaida sana. Mazoezi yametupa nguvu. Wizi na ubakaji wa wazee umepungua. Tumepata pia nguvu za kulima mashamba na kupanda mboga licha ya umri wetu. Tutafunza hata wajukuu wetu kujilinda," anasema Rose Adhiambo, ambae pia ni mwanchama wa Shosho Jikinge.

"Wiki mbili za kwanza tulikua na maumivu makali, kwa sababu ya kufanya mazoezi. Miili yetu imezeeka. Karibu hata tuache kufanya mazoezi."

Beatrice Nyariara, mwanachama wa Jilinde Shoshoo

Wanawake hawa sio kwamba wanajifunza tu kujilinda, lakini pia wana mpango wa kuweka akiba ambao umewawezesha kuwa na biashara ndogo ya kutengeneza mikoba iliyotengenezwa kwa mikono na mapambo ya shanga ambayo wanauza.

"Kila wiki, tunatoa shilingi ishirini za Kenya. Fedha hizi kwa muda sasa zimetuwezesha kutengeza mikoba hii. Angalau tunapata kitu hata kama ni kidogo. Pia, mmoja wetu anapougua au kupata msiba, tunatoa mchango katika akiba yetu na kumsaidia,“ anasema Nyariara huku akionekana mwingi wa mawazo.

Kulingana na makadirio ya polisi nchini Kenya, asilimia 73 ya uhalifu wa kingono hauripotiwi.

Kina mama hao wanasema kwamba kunapokua na tukio au jaribio la wizi au ubakaji polisi na usalama hukawia kufika sehemu ya tukio. Hii ndio sababu yao kuu iliyowafanya kuchukua hatua ya kupata mafunzo ya kujilinda wao wenyewe.

TRT Afrika