Mkutano wa Kilele wa 11 wa Shirika la Merck Africa-Asia Luminary jijini Dar es Salaam, Tanzania, umewakutanisha wake wa marais kutoka zaidi ya nchi 15 za Afrika na Asia kushughulikia masuala muhimu ya afya katika mabara yote mawili.
Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan alifungua mkutano huo, akisisitiza umuhimu wa uwekezaji wa huduma za afya, elimu kwa wasichana, na suluhisho la upishi safi kama njia za kuboresha afya.
Rais Samia alisisitiza juhudi za Tanzania kupanua upatikanaji wa huduma za afya, ambapo zaidi ya hospitali 127 za wilaya na vituo 367 vya afya vimeanzishwa nchi nzima.
"Kuongezeka kwa vituo vya huduma za afya ya mama na mtoto kumesababisha kupungua kwa vifo vya mama na mtoto," alisema, akibainisha kuwa vifo vya uzazi vimepungua kwa zaidi ya 80%, ingawa changamoto bado zipo.
Pengo kubwa, hata hivyo, ni uhaba wa wataalamu waliobobea kusaidia miundombinu hii ya afya inayokua, haja iliyoshughulikiwa kwa kiasi na michango ya Merck Foundation kupitia mafunzo maalumu kwa madaktari nchini Tanzania.
Elimu hasa kwa watoto wa kike ni kipaumbele kingine kwa Rais Samia. "Kama viongozi wanawake, sisi ni uthibitisho wa nguvu ya mabadiliko ya elimu. Kama mwalimu wa zamani, najua elimu ndiyo msingi wa uwezeshaji wa wanawake," alisema.
Mkutano huo ulitoa nafasi kwa Wake wa Marais kubadilishana mawazo ya mikakati ya kuendeleza huduma za afya na elimu na kuondoa fikra potofu kuhusu utasa.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Merck Foundation Prof. Dk. Frank Stangenberg-Haverkamp alizungumza kuhusu uhaba wa wataalamu wa afya barani Afrika, akisisitiza jukumu la shirika hilo katika kutoa elimu maalum kwa madaktari katika mabara yote.
Aliwapongeza Wake wa Marais kwa kuunga mkono kampeni ya “More than a Mother” inayozungumzia fikra potofu ya utasa, elimu ya wasichana na ukatili wa kijinsia.
"Shirika la Merck Foundation inahamasisha jamii kwa ajili ya mabadiliko ya kitamaduni ili kuondoa fikra potofu kuhusu utasa, kuwawezesha wanawake na vijana kupitia elimu, na kutoa suluhisho ya huduma za afya," alisema.
Mke wa Rais wa Zimbabwe, Dkt. Auxillia Mnangagwa, alishiriki jinsi programu za mafunzo za Merck zimepanua utaalamu wa afya na fursa za masomo nchini mwake.
Mke wa Rais wa Kenya, Rachel Ruto, alihimiza kampeni hiyo kujumuisha usalama wa chakula shuleni, akisema, "Sahani ya chakula ni nguvu kwa mtoto."
Mke wa Rais wa Maldives, Madam Sajidha Mohamed, alisisitiza maendeleo ya taifa lake katika mabadiliko ya huduma za afya, akitaja msaada wa Merck kama muhimu katika kushughulikia changamoto kuu za kiafya.
Aliangazia mahitaji yanayoendelea katika maeneo kama vile utunzaji wa saratani na matibabu ya uzazi na akaomba msaada endelevu wa kujenga uwezo wa huduma ya afya.
Mkutano huo wa kilele wa siku mbili unawaleta pamoja mawaziri, watunga sera, wataalam wa afya, na waandishi wa habari kutoka zaidi ya nchi 70 ili kuleta suluhu ya kudumu kwa mustakabali mzuri wa afya barani Afrika na Asia.