Mkutano huo ulifuatia maombi ya Rais wa Uganda Yoweri Museveni./Picha: Yoweri Museveni X

Rais wa Uganda Yoweri Museveni siku ya Jumatano amekutana na mwenzake wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Felix Tshisekedi kwenye ikulu ya Uganda kujadili masuala ya amani.

“Sote tumekubaliana kuwa wanachohitaji Wacongo ndicho tunachohitaji Waganda. Kwa hiyo, tumejadiliana mambo mengi hapa, namshukuru sana mheshimiwa Tshisekedi kukubali mualiko wangu, ” alisema Rais Museveni katika taarifa yake.

Kulingana na taarifa hiyo, Majeshi ya Ulinzi ya Uganda yako katika operesheni ya pamoja na majeshi ya DRC (FARDC) kuwasaka waasi wa ADF, kikundi chenye mahusiano ya karibu na kikundi cha kigaidi cha Daesh ambacho kimekuwa kikishambulia Uganda kutokea mashariki ya Congo.

Ziara ya Tshisekedi inafuatia ziara ya Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa nchini Uganda, ambapo alizungumzia hali tete mashariki mwa Congo.

Eneo la mashariki mwa Kongo imekumbwa na ghasia tangu miaka ya 1990 huku mamilioni ya watu wakiwa wameuawa na wengine wengi kuyakimbia makazi yao kufuatia vita vya wenyewe kwa wenyewe.

TRT Afrika