Watu wapatao watatu walipoteza maisha kwenye ajali hiyo iliyohusisha helikopta ya Jeshi la Ulinzi la DRC./Picha: Agence Congolaise de Presse

Watu wapatao watatu wamepoteza maisha kufuatia ajali iliyohusisha helikopta inayomilikiwa na Jeshi la Ulinzi la DRC (FARDC) jijini Kinshasa siku ya Oktoba 30.

Kulingana na vyanzo vya kijeshi, helikopta hiyo ilipata ajali majira ya asubuhi katika eneo la kurukia la uwanja wa ndege wa Ndolo ulioko jijini Kinshasa.

Abiria wote watatu, akiwemo rubani wa chombo hicho, rubani msaidizi na mhandisi wa helikopta hiyo wamefariki dunia kufuatia ajali hiyo kulingana na vyombo vya habari vya nchi hiyo, vikiongeza kuwa rubani wa helikopta hiyo alibanwa na mkanda wa kiti kwenye helikopta hiyo na kufa papo hapo.

Abiria wengine wawili walifariki dunia wakiwa njiani kufikishwa hospitalini, kulingana na mamlaka ya usalama wa anga ya nchi hiyo (RVA).

Taarifa hizo, pia zilithibitishwa na Jenerali Fae Ngama, kamanda wa FARDC.

Kulingana na Christophe Lomami, meya wa Barumbu, chanzo cha ajali hiyo bado hakijajulikana.

TRT Afrika