Vita dhidi ya usugu wa viini duniani sasa unaangaliwa kwa pamoja, kwa ushirikiano wa sekta za wanyama na wanadamu. / Picha: Reuters

Kifo cha mama yake miaka sita iliyopita kilikuwa mwamko mbaya kwa Saviour Yevutsey.

"Kilichoanza kama kikohozi kidogo kiligeuka kuwa nimonia ," anakumbuka.

"Baada ya dawa kadhaa kusimamiwa bila uboreshaji wa aina yoyote, mama yangu alipewa rufaa ya kwenda hospitali nyingine ya wilaya na baadaye hospitali ya kufundishia kwa matibabu zaidi."

Yevutsey alitumia pesa nyingi kununua dawa ambazo hazikumpa nafuu inayohitajika kwa mama yake na akafa, kumbukumbu ambayo bado inamletea maumivu.

Aligundua kuwa mama yake alikuwa na usugu wa viini, ambayo hutokea wakati vijidudu kama bakteria na virusi vinapokua na uwezo wa kushinda dawa zilizoundwa kuwaua.

Dawa husika ni kama antiseptiki, viua vijasumu yani antibayotiki na dawa za kuuwa vimelea.

Shirika la Afya Duniani linatumia maelezo kutoka kwa walioathiriwa moja kwa moja kama Savior kuelimisha wananchi wengine kuhusu jinsi ya kujikinga na usugu wa viini.

"Kila wakati tunapotumia dawa za kuua viini kutibu maambukizi kwa watu, wanyama na mimea, vijidudu hivi vina nafasi ya kukabiliana na matibabu, na kufanya dawa hizo zisifanye kazi kwa wakati," WHO imesema.

Vita dhidi ya usugu wa viini duniani sasa unaangaliwa kwa pamoja , kwa ushirikiano wa sekta za wanyama na wanadamu.

"Madawa ya viini ni kikundi cha madawa tunatumia kutuponya magonjwa ya viini kama bakteria ama virusi ama wadudu. Usugu unatokana wakati vile viini ama virusi haviskii ile dawa, unakuta dawa haiponyi ama haimalizi magonjwa," Dkt. Victor Yamo ameambia TRT Afrika.

Kutowapa wanyama mazingira masafi na lishe bora kutapelekea wawe wagonjwa na dawa ambayo wanapewa itajipata katika chakula kama nyama, maziwa ambayo wanadamu wanapata kutoka kwa wanyama/ picha: Reuters 

Dkt. Victor Yamo ni meneja wa Kampeni za Kilimo Endelevu za Kibinadamu katika shirika la World Animal Protection.

"Hii inatokana kwa sababu yale matumizi ya dawa yamekuwa si ya hali ya juu ama inavyofaaa sasa virusi vimezoea hiyo dawa na kutibu mtu au mnyama itahitaji dawa nyingine au dawa ya hali ya juu," Dkt Yamo anasema.

Kila mwaka kuanzia tarehe 18 hadi 24 Novemba, Jumuiya ya kimataifa huadhimisha wiki ya Uhamasishaji na kampeni dhidi ya usugu wa viini.

Hii ni kwa nia ya kuongeza ufahamu wa hatari zinazoletwa na matumizi yasiyofaa ya dawa za kuuwa viini na virusi na vimelea kwa binadamu, wanyama na mimea.

Usugu kutoka shambani

Usugu wa viini unaweza kupata kutoka kwa wanyama kama wanadamu.

"Kwa kawaida tunataka kumpa mnyama chakula bora na maji masafi lakini unakuta saa zingine mahindi yameharibika kidogo, hiyo ndiyo tunachowalisha ngombe au kuku nayo, na hayo ni makosa , " Dkt Yamo amesema.

Dr. Victor Yamo, mtaalmu kutoka World Animal Protection anasema mara mingi wakulima huchanja wanyama wakati ambao haufai na hiyo dawa hupitishwa kwa wanadamu kupitia maziwa na nyama/  picha kutoka World Animal Protection

"Pili unakuta pale mazingira ambapo wanyama walipo si masafi, unaweza kukuta panya au ndege wa porini wameingia hapo na kuleta magonjwa, Hii inamaanisha tutawapa dawa na hiyo dawa itapatikana katika chakula ambayo mwanadamu atakula , kama mayai, maziwa, nyama na kisha itamdhuru."

Wataalamu wanasema kuwa mkulima kujiamulia dawa ya kuwapa mifugo yake bila kuomba mwongozo wa dakitari wa wanyama huenda ikapeleka awape wanyama dawa isiyofaa na hii dawa itapatikana kwenye chakula ambacho mwanadamu atachukua kutoka kwa wanyama hao.

"Makosa mengine ni kuwa wakati wanyama wanakuwa wagonjwa tunaenda kuuliza jamaa na majirani kuhusu dawa za kuwapa, nao wanatueleza dawa waliyotumia ilhali labda siyo inayofaa," Dkt Yamo ameambia TRT Afrika.

"Kitu kingine ni kuwa wakati tumepewa dawa tukipata nafuu au wanyama wakipata nafuu tunawaacha kuendelea na hiyo dozi, tunachagua kuwaacha kuendelea na hapo basi viini vinavyobaki vina ususuu. Ugonjwa ukirudi hauwezi kutibiwa na ile dawa ama inabidi dozi iongezwe."

TRT Afrika