Mifumo dume au wakibaguzi wa kijinsia iliyokita mizizi, upendeleo na mitazamo inaathiri uwezo wa wasichana na wanawake vijana kutumia mitandao, kuathiri shughuli zao za mtandaoni na kuathiri ufikiaji wao wa habari na kazi, ripoti mpya imebaini.
Utafiti wa watumiaji zaidi ya 10,000 wenye umri wa miaka kati ya 14-21, na wazazi wao, katika zaidi ya nchi sita zikiwemo Ethiopia, Kenya, Nigeria, Tanzania na India, uligundua kuwa wasichana wanafuatiliwa kila mara na kuambiwa kuwa wako katika mazingira magumu na hawana uwezo mtandaoni, " na hivyo kusababisha mazingira ya kutojiamini."
"Hii inasababisha wasichana kuweka kinga zaidi na kuwa na tabia ya kihafidhina wanapoungana na wengine na kushiriki habari za kibinafsi mtandaoni," ilisema ripoti ya shirika lisilo la kiserikali la Girl Effect, Mfuko wa Malala, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF na wakfu wa Vodafone Americas.
"Mitazamo hii haiathiri tu upatikanaji na matumizi ya mitandao kwa wasichana, inaathiri kujiamini kwao na kuunda mitazamo yao wenyewe ya uwezo wao wa kutumia zana hizi kutekeleza masilahi yao ya kijamii, kielimu na kiakili," iliongeza ripoti hiyo.
Mgawanyiko wa kidijitali wa kijinsia umeendelea licha ya juhudi za serikali duniani kote. Utafiti wa UNICEF mapema mwaka huu ulionyesha kuwa katika nchi 54, uwiano wa wastani wa usawa wa kijinsia ni 71, ikimaanisha kuwa kwa kila vijana 100 wa kiume wanaotumia mtandao wa intaneti, ni wasichana 71 pekee wanaotumia mtandao.
Wakati huo huo, wanawake hupata unyanyasaji zaidi mtandaoni, na unyanyasaji unawasukuma wasichana kuacha majukwaa ya mitandao ya kijamii kama vile Facebook na Instagram, tafiti za hivi majuzi zimegundua.
Miongoni mwa vijana waliounganishwa kidijitali, asilimia 12 zaidi ya wasichana kuliko wavulana walisema kuwa wanahisi kujijali wanapotumia mitandao ya kijamii, na wana uwezekano mdogo wa asilimia 11 kutuma picha au maoni mtandaoni ikilinganishwa na wavulana wa umri huo, ripoti ya Girl Effect iligundua.
Kwa vile utumiaji huru wa wasichana wa mtandao unazuiliwa na upendeleo na hofu ya unyanyasaji, hawajioni kama wataalam wa teknolojia, na hawaoni mtandao kama kitu ambacho ni chao, ripoti kutoka Girl Effect ilisema.
Ujuzi wa kidijitali
"Hii inaleta mzunguko mbaya ambapo wasichana huepuka teknolojia kwa sababu hawaoni kuwa wanastahili na kisha teknolojia inaonekana kama 'sio yao' kwa sababu wamekuwa wakiepuka," ilisema.
Kama vijana ambao hujichunguza na kujidhibiti miendendo yao mtandaoni, wanawake "mara nyingi hubeba sifa hizi hadi mahali pao pa kazi, ambapo wanakabiliwa na matatizo katika kuonyesha ujuzi wao na kujenga uhusiano wa kimkakati," alisema Mitali Nikore, mtaalamu wa sera za jinsia katika kikundi cha utafiti cha Nikore Associates.
"Hii inaathiri vibaya tabia ya wanawake katika maeneo ya kazi, ikizuia fursa zao za soko la ajira na maendeleo ya kitaaluma na upatikanaji wao wa vyanzo vinavyowezekana vya shughuli za kuzalisha mapato," Nikore aliiambia Wakfu wa Thomson Reuters.
Kando na upatikanaji bora wa simu mahiri kwa wasichana na wanawake vijana, programu za kusoma na kuandika dijitali na kukomesha ubaguzi unaozingatia kanuni za kijinsia zinahitajika, alisema Nikore.
Sheria ziko nyuma
Wasichana lazima pia washirikishwe katika kuunda bidhaa za kidijitali kwa mahitaji yao, alisema msemaji wa shirika la Girl Effect.
Kwa mfano, Girl Effect ilitengeneza chatbots zilizowezeshwa na akili bandia nchini Afrika Kusini na India - Big Sis na Bol Behen ("niambie, dada") - pamoja na wasichana, kama chanzo cha taarifa sahihi kuhusu afya ya jumla na ustawi wa afya ya uzazi kwa wasichana.
Ingawa sheria mpya kama vile Sheria ya Usalama ya Mtandaoni ya Uingereza na Sheria ya Usalama ya Watoto Mtandaoni inayopendekezwa nchini Marekani inaweza kusaidia kuwalinda watoto kwa kiasi fulani, "kanuni zinaweza tu kusaidia kiwango fulani, na mara nyingi zibaki nyuma ya maendeleo ya teknolojia," msemaji wa Girl Effect alisema.
"Wasichana vijana na wanawake vijana wanataka kuhusika katika kuunda suluhu; wana mawazo wazi kwa ajili ya kazi, uzoefu, na mikakati ambayo inaweza kutumika kufanya mtandao kuwa mahali salama na kufikiwa zaidi."