Klabu ya Wolverhampton Wanderers inayoshiriki Ligi Kuu ya Uingereza imetoa pendekezo la kufuta matumizi ya VAR, kuanzia msimu ujao wa 2024-25.
Hatua hiyo itazilazimu klabu zinazoshiriki Ligi Kuu ya Uingereza kupiga kura maalumu katika mkutano wao ujao, ili kuondoa VAR kwenye msimu ujao wa Ligi hiyo, maarufu kama EPL.
Hata hivyo, katika miaka ya hivi karibuni, maamuzi ya VAR yamepata malalamiko makubwa kutoka kwa vilabu na mashabiki wa soka kwa ujumla duniani.
Kwa sasa, azimio la kupitisha maamuzi hayo limepelekwa kwenye uongozi wa ligi ya EPL na klabu ya Wolverhampton Wanderers, hatua itakayolazimisha upigwaji wa kura kutoka kwa wawakilishi 20 wa klabu za zinazoshiriki Ligi Kuu ya Uingereza, katika mkutano wao utakaofanyika, Juni 6 mwaka 2024, katika mji wa Harrogate nchini Uingereza.
Katika taarifa yake, klabu ya Wolves imesema kuwa imezingatia na kufanya tathmini kubwa na kusisitiza kuwa bado inaheshimu Chama cha Waamuzi wa katika Ligi Kuu ya Uingereza (PGMOL).
“Hakuna haja ya lawama, tunatafuta njia sahihi ya kuokoa mpira wetu na wadau wengine wamefanya jitahada zaidi kufanikisha hili," taarifa hiyo imesema.