Dkt Wliibrod Slaa amewahi kuwa Balozi wa Tanzania katika nchi mbalimbali zikiwemo  Sweden, Denmark, Finland na Norway./Picha: Wengine

Mwanasiasa mkongwe nchini Tanzania Dkt Willibrod Slaa, amefikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kujibu shitaka la kusambaza taarifa za uongo katika mtandao wa X (zamani Twitter).

Mwanadiplomasia huyo ambaye amenyimwa dhamana kwa sababu za usalama wake, anakabiliwa na shitaka la kukiuka Kifungu cha 16 cha makosa ya kimtandao.

Mapema siku ya Januari 10, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro alithibitisha taarifa za kushikiliwa kwa mwanadiplomasia huyo.

Dkt Slaa alisomewa mashitaka yake mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Beda Nyaki ambapo alidaiwa kutenda kosa hilo chini ya kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Kimtandao namba 14 ya mwaka 2015.

“Upande wa Jamhuri umepeleka kiapo mbele ya Mahakama cha kupinga Dkt Slaa asipewe dhamana kwa sababu wanachoiita usalama wake…kiapo hiko hakikutolewa kwa mawakili wa upande wa pili,” alieleza Boniface Mwabukusi, ambaye pia ni Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS).

Kulingana na Mwabukusi, dhamani ni haki ya mtuhumiwa na haikuwa vyema kumnyima Dkt Slaa dhamana, hasa kutokana na nafasi yake nchini Tanzania.

Mbunge huyo wa zamani wa Jimbo la Karatu nchini Tanzania, anadaiwa kuandika ujumbe kupitia akaunti ya Maria Sarungi @MariaSTsehai alindika ujumbe uliosomeka:

“Wakubwa wametafutana, nikasema wakubwa namaanisha Mwamba na Samia, na wala hatuna maneno ya kumung’unya…na kimsingi wamekubaliana Suluhu Samia amekubali atatoa pesa, Suluhu Samia amekubali ataongeza nguvu ya pesa ni dhahiri atatoa pesa…hizo ni hela za Watanzania wanazichezea Samia na watu wake.”

Mahakama hiyo imeahirisha shauri hilo mpaka siku ya Jumatatu, Januari 13.

TRT Afrika