Magdalena Shauri ameshiriki mashindano mbalimbali ya ndani na nje ya nchi na kufanikiwa kupata medali.

Na Suleiman Jongo

Shirikisho la Riadha nchini Tanzania (RT) limempongeza mwanariadha wake wa kike Magdalena Shauri kwa kushinda nafasi ya tatu ya michuano ya riadha ya Berlin Marathon iliyofanyika huko Berlin na kufuzu michuano ya Olimpiki ya Paris.

Madgalena ametumia muda wa 2:18:40 na kwa ushindi huo amekata tiketi ya kushiriki michuano hiyo ya Olympic itakayofanyika Paris mwakani. Ameweka tofauti ya dakika 7 na mshindi wa kwanza, Tiggist Assefa kutoka Ethiopia.

Kaimu Katibu Mkuu wa RT ambaye pia ni mwanasheria kitaaluma, Otte Ndaweka amesema wanajivunia sana kwa rekodi nzuri iliyowekwa na Shauri na kupeperusha vema bendera ya Tanzania.

”Tunaelewa ushindani ulikuwa ni wa hali ya juu sana, hivyo kwetu sisi ushindi wake ni sehemu ya mafanikio,”amesema.

Shauri mpaka sasa anakuwa mwanariadha wa tatu wa mbio ndefu kutoka Tanzania waliofuzu kwa ajili ya michuano ya Olimpiki.

Wengine ni mwanariadha maarufu Alphonce Simbu, anayejivunia medali mbalimbali, ikiwemo ya Mumbai Marathon mwaka 2017 na kumaliza nafasi ya tano katika michuano ya Olimpiki ya mwaka 2016.

Mwingine ni Gabriel Geay, anayejivunia rekodi mbalimbali za kimataifa, ikiwemo ya kushinda nafasi ya pili katika michuano ya Boston Marathon ya mwaka huu.

“Mikakati mingine ni kuhakikisha wanariadha wetu wa kimataifa wanavuka mipaka ya nchi na kwenda kushiriki katika mbio mbalimbali za kimataifa ili waweze kujiwekea mazingira ya kufuzu.”

Kaimu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Riadha Tanzania Otte Ndaweka

Kwa mujibu wa Ndaweka, RT imejiwekea mipango mbalimbali kuhakikisha wanaridha wengi kutoka Tanzania wanafuzu kwa ajili ya michuano hiyo ya Olimpiki na kujiwekea nafasi ya kushinda medlai kama ilivyo kwa nchi jirani ya Kenya.

“Wiki inayo tumeandaa michuano maalumu ya kitaifa katika mkoa wa Morogoro kwa ajili ya kuendelea kutafuta wanariadha wanaoweza kufuzu kwa ajili ya michuano ya Olimpiki.”

“Mikakati mingine ni kuhakikisha wanariadha wetu wa kimataifa wanavuka mipaka ya nchi na kwenda kushiriki katika mbio mbalimbali za kimataifa ili waweze kujiwekea mazingira ya kufuzu,”

”Na mmoja wapo ni Sarah Ramadhani, ambaye siku chache zijazo atasafiri kwenda nchini Japan kushiriki michuano ya Nagai Marathon,” amesema.

Tanzania imeanza kushiriki michuano ya Olimpiki toka mwaka 1964 na imefanikiwa kushinda medali mbili tu za fedha kupitia wanariadha wa zamani Filberti Bayi na Suleiman Nyambui.

Ushiriki wa idadi ndogo ya wanamichezo na ufinyu wa bajeti ni moja ya sababu ya kufanya vibaya, ukilinganisha na nchi nyingine kama Kenya.

Katika mbio za wanawake za Berlin zilizofanyika alfajiri ya leo, Muethiopia Assefa amevuka mstari na kuwa mshindi wa kwanza kwa kutumia muda wa saa 2:11:53.

Kwa upande wa wanaume, mwanaridha mkongwe Eliud Kipchoge raia wa Kenya ameibuka mshindi wa michuano hiyo akitumia muda wa 02.2.42.

Hii ni mara ya tano kwa Kipchoge kushinda michuano hii ya Berlin Marathon, iliyovutia wanariadha kutoka mataifa mbalimbali ulimwenguni.

TRT Afrika