Waziri wa Kilimo nchini Tanzania Hussein Bashev

Waziri wa Kilimo nchini Tanzania amesema serikali imechukua hatua kadhaa kuhakikisha uhaba wa tatizo la sukari nchini linaondoka haraka iwezekanavyo. Hussein Bashe ambae ni Waziri wa Kilimo nchini humo amesema kuwa, miongoni mwa hatua hizo, ni pamoja na kutoa vibali vya kuruhusu uingizaji wa sukari wa takriban tani laki moja kutoka nje.

Kauli hii ya serikali, inakuja baada ya bidhaa hiyo muhimu kupanda bei kutoka shilingi elfu mbili hadi elfu nne na katika baadhi ya maeneo kuadimika kabisa. Hali ambayo inaonekana kuibua wasiwasi miongoni mwa wananchi kutokana na umuhimu wa matumizi ya bidhaa hiyo ambayo mahitaji yake kwa siku nchini humo ni takriban lakini 1500.

"Hatua ya kwanza tuliyochukua kama serikali, ni kuruhusu uagizaji wa sukari wastani wa tani laki moja ambao tumewapa viwanda ili waweze kuingiza hiyo sukari, maamuzi ya kuwapa viwanda sio ya bahati mbaya, kama mnavyofahamu, ni lazima tulinde viwanda vyetu vya ndani, na hatulindi kwa gharama ya mlaji, bei ya sukari kabla ya tatizo hili, viwandani ilikuwa 2240 mpaka 2270 na bei ya reja reja ilikuwa inatembea kati ya 2700 mpaka 3000, leo imepanda baadhi ya maeneo mpaka kufika 4000. Serikali tumewaagiza wenye viwanda kuhakikisha kwamba wanasimamia usambazaji wao kama kawaida bila kumuumiza mlaji. Lakini hatua ya pili tuliyochukua serikali, tumetoa idhini ya uagizaji wa sukari zaidi ya tani laki moja, tunaamini hii ikiingia katika mfumo wetu wa ugavi, hali ya usambazaji wa sukari itakuwa nzuri," amesema Bashe.

Tanzania ina jumla ya viwanda saba vya sukari, vikubwa kati ya hivyo ni Kilombero, ambayo kwa siku inazalisha tani 700 za sukari, hata hivyo kiwango kimeshuka hadi 250, TPC kwa siku tani 450 lakini kwa sasa kimesimamisha uzalishaji kutoka na hitilafu za mashine, huku Kagera Sugar ikiwa na uwezo wa kuzalisha tani 500 kwa siku, lakini sasa inazalisha wastani wa tani 200 hadi 300. Viwanda vyengine ni Mtibwa na Bagamoyo, ambapo kwa mujibu wa serikali, kutokana na mvua kubwa zinazoendelea, uzalishaji umepungua kwa takriban tani elfu moja kwa siku.

Waziri huo amefafanua kuwa, katika kipindi cha mvua, mbali na uvunaji na uchakataji wa sukari unavyokuwa mgumu, lakini kiwango pia cha sukari katika miwa kinapungua kwa zaidi ya asilimia 25.

TRT Afrika