Na
Firmain Mbadinga
Pinocchio, shujaa mkuu wa riwaya ya hadithi ya mwandishi wa Italia Carlo Lorenzini inayoitwa The Adventures of Pinocchio, huenda amekuja kuwa hai katika kubuni, lakini viumbe vya mbao vya Sorobabel Ntutumu Obono vinaleta uhai katika nyumba nyingi nchini Equatorial Guinea.
Ingawa havitembei wala kuongea, viumbe vya Sorobabel Ntutumu Obono mwenye umri wa miaka 30 vimejaa uhai, na rangi zao na maumbo ni kivutio cha kweli kwa yeyote anayepata nafasi ya kuviona au kuvigusa huko Bata, mji mkuu wa kiuchumi wa nchi hio ya Afrika Magharibi.
Iwe ni mti wake wa vikombe wenye samaki aina ya sangara miguuni mwake, au kikapu chake cha matunda ambacho mahindi, maboga na maharage yanaishi kwa pamoja, au kikapu chake cha vyakula vya baharini ambacho kaa, prawns na lobster vinashindana kwa kung'ara, Sorobabel hutengeneza vitu hivi vya mapambo vya nyumbani kwa jicho la kina linalovifanya viwe hai zaidi.
"Nikihamia tena Bata kutoka kijijini mwangu mnamo 2006, nilikuwa tayari nimehamasika na nilikuwa na hamu ya kuwa mchongaji au fundi stadi. Hata wakati wa masomo yangu na kazi za hapa na pale nilizofanya, ilikuwa inaishi ndani yangu, na nilijua siku moja nitatimiza hamu yangu ya kuweka msukumo wangu wa ubunifu katika vitendo," Sorobabel anasimulia TRT Afrika kuhusu motisha yake ya maisha.
Kabla ya kuitikia wito wa nyundo ambayo sasa ni zana yake kuu ya kazi, Sorobabel alikuwa na fursa ya kuthibitisha uwezo wake kama fundi teknolojia na ufundi katika wilaya yake ya nyumbani ya Mofono yemfen Evinayong.
Uzoefu wake katika biashara hizo mbili uliimarisha ustadi wa mikono wa Sorobabel, kabla hajajitolea kuonyesha sanaa yake kwenye mbao mwaka wa 2018.
"Baada ya uzoefu huu wa kitaaluma, nilirudi kwa wazazi wangu wanaoishi Bata na nikaanza kujihusisha na sanaa. Kwa hivyo, nilikuwa na mawazo mengi kuhusu mbao na siku moja nilisema lazima niyaweke haya katika vitendo."
"Nilianza kidogo kidogo na vikombe vya mianzi, na kutoka hapo nilianza kupata msukumo kutoka kwa wengine, nikijaribu kila mara kuweka ustadi zaidi katika viumbe vyangu." anasema kwa TRT Afrika.
Ili kuongeza ustadi wa vitu hivyo, fundi huyo pia anatumia sander ya umeme, ambayo inatumika kung'arisha mbao na chuma.
Alipoanza kwanza, Soro, kama anavyojulikana na wale walio karibu naye, anasema kwamba kulikuwa na hamasa na moyo mdogo kutoka kwa raia na kuamini ufundi wake kuliko ilivyo leo.
Msanii huyo amegeuza kile alichokiona kama tofauti kuwa chanzo cha motisha ya kutengeneza vitu vizuri zaidi na kuboresha mauzo yake.
"Ilinifanya niwe na nguvu zaidi na nilitaka kufanya kazi kwa bidii na kuboresha kazi yangu, kwa hivyo, nilianza kupost bidhaa zangu kwenye Facebook na kwenye makundi ya WhatsApp, na kidogo kidogo nikaanza kupata wateja."
"Uzoefu wangu, msukumo, na uvumilivu na kazi unaendelea kukua siku hadi siku. Kadri muda unavyopita, ninakuwa na nguvu zaidi na kupata msukumo zaidi wa kutengeneza mifano mingine ambayo ni tofauti kabisa na ile niliyotengeneza hapo awali," kijana huyo kutoka Guinea ya Ikweta anaeleza kwa sauti yenye kujiamini.
Kwa kazi zake zote za ubunifu hadi leo, hata kama kazi ya kwanza ilikuwa ile iliyomweka chini ya msongo wa mazwazo, Sorobabel anasema hana upendeleo.
"Hadi leo hii, uzoefu wangu, msukumo, maslahi, na amani na kazi yangu inaendelea kukua kila siku, na ninafanya kila niwezalo kujituma hadi sentimita ya mwisho ili kutoa kazi yenye ubora daima ili kila kitu kiwe na faida," anaeleza Sorobabel, ambaye kazi yake inazidi kuzua heshima na udadisi zaidi.
Kama ilivyo katika nchi nyingi za Afrika, soko la sanaa nchini Equatorial Guinea lina wateja wa aina mbalimbali.
Mbali na Wa-Guinea wenyewe, wateja wa kigeni ndio kwa sasa wanaoweka oda nyingi zaidi kwa wasanii kama Sorobabel Ntutumu Obono.