Vikosi vya usalama vya Somalia siku ya Jumatatu vilinasa akiba ya silaha zinazodaiwa kutoroshwa kutoka taifa jirani.
Serikali ya Somalia ilisema silaha hizo zilitoroshwa kutoka mji wa mpakani na "wauzaji wa silaha wasio waaminifu."
Kulingana na wizara ya mambo ya ndani ya nchi hiyo, "wanamgambo wenye silaha" walivizia jeshi wakati wa kunyakua silaha hizo, ambazo zilikuwa zikibebwa kwenye lori.
Machafuko hayo yalisababisha "baadhi ya silaha zilizonaswa kuangukia mikononi mwa waasi," serikali ya Somalia ilisema katika taarifa yake siku ya Jumanne.
"Serikali ya Somalia inalaani vikali vitendo vya kuchukiza vya wanamgambo waliothubutu kushambulia jeshi letu la taifa, ambalo lilikuwa likitekeleza wajibu wake kwa uwajibikaji," serikali ilisema.
Somalia iliongeza kuwa biashara haramu ya silaha imechangia pakubwa ukosefu wa usalama nchini humo, ambapo kundi la kigaidi la al-Shabaab linatishia usalama mkubwa.
"Tuko thabiti katika dhamira yetu ya kurejesha silaha zilizoibwa na tutaweka hatua kali za adhabu kwa wale waliohusika katika ghasia hizi mbaya," Somalia ilisema.
Kundi la kigaidi la Al-Shabaab, ambalo limefanya mashambulizi nchini Somalia na mataifa jirani kwa miaka mingi, limeua maelfu ya watu katika kipindi hicho.
Nguvu ya kundi hilo hata hivyo imepungua hivi karibuni huku vikosi vya usalama vya Somalia na kanda vikiendelea na operesheni kubwa ya usalama dhidi ya magaidi hao.