Mchezo wa marudiano ya raundi ya pili ya ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Simba na Power Dynamos umemaliza katika uwanja wa Azam Complex kwa matokeo ya1-1.

Historia ya soka imeandikwa nchini Tanzania kwa vilabu viwili pinzani kufuzu pamoja hatua ya Makundi ya ligi ya Mabingwa Barani Afrika baada ya Simba leo Oktoba 1, 2023 kuwatoa Power Dynamo ya Zambia kufuatia sare ya 1-1.

Simba wao wamefuzu kwa faida ya bao la ugenini baada ya kutoka sare ya 2-2 katika mechi ya kwanza iliyochezwa katika uwanja wa Levy Mwanawasa takriban wiki mbili zilizopita.

Hivyo, sare ya 1-1 ya leo Oktoba 1, 2023 katika uwanja wa Chamazi jijini Dar es Salaam haikutosha kuibeba Power Dynamo, licha matokeo ya jumla (aggregate) kuwa 3-3.

Andy Boyeli alianza kuifungia Power Dynamo dakika ya 16, goli ambalo lilidumu hadi mapumziko.

Simba, ilianza kipindi cha pili kwa nguvu, ambapo nahodha John Bocco aliyeingia kipindi cha pili aliachia mkwaju mkali dakika ya 69 uliopelekea beki wa Dynamo Kondwani Chiboni kujifunga na kuipa Simba goli muhimu.

Hivyo, vilabu vya Simba na Yanga ambavyo ni mahasimu kwa pamoja vinafuzu hatua ya makundi.

Wakati Simba kwa zaidi ya misimu minne ikifuzu hatua hii, Yanga wao mara ya mwisho walifuzu mwaka 1998.

TRT Afrika