Na Suleiman Jongo
Katika kile kinachoonekana kuwa mashabiki wa Simba hawafurahishwi na kiwango cha timu yao licha ya kufuzu hatua ya makundi ya ligi ya Mabingwa Barani Afrika, uongozi wa Simba nchini Tanzania umetoa majibu kuwa watayafanyia kazi mapungufu yote kabla ya kukutana na timu hizo vigogo katika hatua hiyo ngumu.
Simba imefuzu hatua ya makundi kwa faida ya bao la ugenini, bao ambalo hata hivyo, inaonekana kwa baadhi ya mashabiki kuwa walilipata kama bahati baada ya beki wa Power Dynamo ya Zambia Kondwani Chiboni kujifunga mwenyewe.
Hali hii ilionekana kuwavuruga mashabiki, akiwemo rais wa heshima na mwekezaji Mohamed Dewji, ambaye alizua mjadala katika mitandao ya kijamii baada ya kuandika ujumbe huu, “Dah, jamani Simba mtaniua kwa presha."
“Tunawaomba washabiki waendelee kutuunga mkono. Katika football mambo mengi yanatokea na sio kila siku utakuwa na furaha. Mashabiki wasikate tamaa na sisi tunaendelea kupambana. Sisi kama wachezaji, tayari tumemaliza na tunajiandaa na hatua ya makundi. Muhimu tumefuzu na mengine yatakaa sawa katika siku za usoni.”
Mashabiki kadhaa walionekana kulinyooshea kidole benchi la ufundi likiongozwa na Mbrazil Roberto Oliveira, huku wengine wakionekana kutofurahishwa na namna mabingwa hao wa zamani wanavyocheza, licha ya kuwa na kikosi kipana chenye wachezaji 12 wa kigeni.
Akiongea baada ya mechi ya marudiano iliyomalizika kwa sare ya 1-1 jijini Dar es Salaam, Mtendaji Mkuu wa klabu ya Simba Imani Kajula amesema wana muda wa kutosha kufanyia kazi maeneo yanayoonekana kuwa na shida, huku akikiri kuwa hata hivyo mechi zao zote mbili dhidi ya Power Dynamo zilikuwa ni ngumu sana.
“Tulijua tuna wapinzani wazuri sana toka tulipokuwa Zambia katika mechi yetu ya kwanza baada ya kutoka sare ya 2-2 na baadae kupata tena sare ya 1-1 jijini Dar es Salaam.“
“Power Dynamo ni timu nzuri na siyo timu nyepesi na walishawahi kuwa hata mabingwa wa kombe la Shirikisho Barani Afrika.“
“ Tumesahau ya nyuma na tutafanya maboresho ili kuelekea katika makundi.“
“Tuna kazi ya kufanya katika kuboresha kikosi chetu.“
“Jambo hili ni muhimu kwa sababu tuna mechi ngumu mbele yetu,“
“Tunajiandaa pia na African Super League na tutakutana na Al-Ahly ya Misri tarehe 20,”
“Hivyo, tunajua kuwa tuna kazi ngumu mbele yetu,“
“ Lakini tuna amini kuwa tuna muda wa kutosha kuweka mambo sawa,“ amesema Kajula.

Mashabiki kadhaa wameonekana katika mitandao ya kijamii wakikosoa namna timu yao ilivyohaha kufuzu, tofauti na misimu mingine iliyopita.
Katika kile kinachoonekana kuendelea kuwapa moyo mashabiki, mmoja wa wachezaji wa Simba ambaye ni mfungaji bora wa msimu uliopita , Saido Ntibazonzika, ambaye ni raia wa Burundi amesema licha ya ukosoaji huo, wachezaji wamepambana na kila mechi wanaipa uzito.
“Wana Simba bado wana furaha na waendelee kutuunga mkono mwanzo hadi mwisho na wasikate tamaa wa kwa sababu hivi ndivyo mpira wa miguu ulivyo,“
“Kuna baadhi ya mashabiki walimzomea Bocco ( John), lakini baadae Bocco huyo huyo ndiye aliyesababisha kupata goli la kusawazisha baada ya kupiga shuti kali na mlinzi wa Power Dynamo kujifunga,“ amesema winga Ntibazonkiza.
“ Hivyo Tunawaomba washabiki waendelee kutuunga mkono,“
“Katika football mambo mengi yanatokea na sio kila siku utakuwa na furaha,“
“Mashabiki wasikate tamaa na sisi tunaendelea kupambana,“ amesema.
“Sisi kama wachezaji, tayari tumemaliza na tunajiandaa na hatua ya makundi,“
“Cha muhimu tumefuzu na mengine yatakaa sawa katika siku za usoni,“ amesema.
Ukiachia mbali kufuzu hatua ya Makundi, Simba ni timu pekee kutoka nchini Tanzania ambayo itashiriki michuano ya African Football League ( Super League iliyoanzishwa na Shirikisho la soka Afrika (CAF).
Simba itacheza na vigogo wa Afrika Al-Ahly katika hatua ya Robo Fainali Oktoba 20, 2023 na marudiano ya mechi hii itakuwa Cairo, Misri Oktoba 24, 2023.
Hii ni michuano mipya barani Afrika inayoshirikisha timu nane na kutoka Tanzania Simba ndio timu pekee kwa sasa. Afisa Habari wa Simba Ahmed Ally amesema kizuri kuna miezi mitatu kuelekea hatua ya makundi, hivyo lazima kazi kubwa ifanywe na benchi la ufundi ili kiwango cha timu kiongezeke. Amesema wametimiza malengo ya klabu kufuzu hatua ya Makundi na mengine yatafuata.
Ukiachia mbali Simba na Al-Ahly, timu nyingine zitakazoshiriki michuano hii ni Mamelodi Sundowns ya Afrika ya Kusini, Waydad Casablanca ya Morocco, Esperance ya Tunisia, TP Mazembe kutoka Jamhuri ya watu wa Kongo [ DRC), Petro Atletico ya Angola na Enyimba ya Nigeria.