Waziri wa mawasiliano  Chernor Bah  pia aliwahakikishia wananchi kuwa vyombo vya serikali viko thabiti na vimedhibiti hali katika taifa./Picha : Reuters 

Amri ya kutotoka nje kwa nchi nzima imetangazwa nchini SierraLeone baada ya milio ya risasi kusikika katika mji mkuu Freetown Jumapili asubuhi. Wizara ya habari inasema watu wenye silaha walijaribu kuingia kwenye kambi ya Wilberforce lakini wakafukuzwa.

Taarifa kutoka kwa wizara ya mawasiliano iliyochapishwa katika mtandao wa X, zamani Twitter, ilisema kuwa watu ambao bado hawajatambuliwa walijaribu kuvamia kwa silaha kambi ya kijeshi Wilberforce lakini walidhibitiwa na kuweza kutimuliwa.

''Katika saa za alfajiri, watu waloijaribu kuvunja ifadhi ya silaha katikakambi ya Wilberforce, lakini wametibuliwa,'' ilisema taarifa iliyowekwa saini na waziri wa mawasiliano Chernor Bah.

Waziri Chernor pia aliwahakikishia wananchi kuwa vyombo vya serikali viko thabiti na vimedhibiti hali katika taifa.

Taarifa hiyo ya Waziri Chernor pia iliwataka watu kufuatilia habari katika vyombo rasmi vya habari vya serikali na kuepukana na madai potofu.

Muda mfupi baada ya taarifa ya waziri Chernor, Rais Julius Maada Bio alichapisha ujumbe katika Twitter akisema ''Amani ya taifa letu tunayoipenda ni ya ajabu na tutaendelea kulinda amani na usalama wa Sierra Leone dhidi ya vikosi vinavyotaka kupunguza utulivu wetu unaothaminiwa sana.''

Rais Bia pia alisisitiza kuwa demokrasia ya taifa itaendelea kuhifadhiwa.

''Tunasalia thabiti katika azimio letu la kulinda demokrasia nchini Sierra Leone na ninawaomba wananchi wote wa Sierra Leone kuungana kuelekea wajibu huu wa pamoja,'' aliongeza Rais Bia.

Sierra Leone ilitangaza Rais Julius Maada Bio kama mshindi wa uchaguzi kwa kura 56% mwishoni mwa mwezi Juni katika kura iliyogubikwa na madai ya ulaghai kutoka kwa upinzani.

Mpinzani wake mkuu Samura Kamara aliibuka wa pili kwa 41% ya kura, kulingana na matokeo ya mwisho yaliyotangazwa na mkuu wa tume ya uchaguzi.

TRT Afrika