Kiongozi wa Uganda Yoweri Museveni amemteua mwanawe kuwa Mkuu wa Ulinzi wa nchi hiyo, serikali hiyo ya Afrika Mashariki ilitangaza, huku ikiongeza utata katika teuzi za Muhoozi Kainerugaba.
Tangazo hilo lililotolewa na Wizara ya Ulinzi Alhamisi jioni, lilifuatia uvumi uliokuwa ukienea kwa miaka mingi kwamba Kainerugaba, ambaye matamshi yake katika mitandao ya kijamii yalizuwa mvutano ya kidiplomasia alikuwa anaandaliwa kuchukuwa nafasi ya baba yake.
Hata hivyo, Jenerali huyo wenye miaka 49, hapo awali alikana tuhuma kuwa anataka kuchukua nafasi ya baba yake, akiwa ni mmoja wa viongozi waliokaa muda mrefu zaidi barani Afrika, na aliyefurahia kupanda ngazi katika safu ya jeshi la nchi hiyo.
Matamshi yake yaliyofutwa kwenye mtandao wa “X” Kainerugaba alisema atawania urais katika uchaguzi wa mwaka wa 2026.
Matamshi makali ya Jenerali Kainerugaba
Pia alionekana akimkejeli baba yake, kwa kuandika: "Ni wangapi wanakubaliana nami kwamba wakati wetu umefika? Inatosha wazee kututawala. Wanatutawala. Ni wakati wa kizazi chetu kung'aa,’’ aliandika katika ukurasa wake wa X huku akiwashawishi wengine kuisambaza taarifa hiyo.
Wizara ya Ulinzi ya Uganda ilitangaza kumpandisha cheo Kainerugaba pamoja na kuwapandisha vyeo maafisa wengine.
Kufuatia mzozo mwaka wa 2022 kuhusu chapisho la Kainerugaba akitishia kuivamia Kenya, Museveni, 79, alimdhibiti mwanawe kwa kumwambia ajiepushe na mitandao ya kijamii linapokuja suala la nchi.
Museveni, ambaye aliomba radhi kwa Kenya kutokana na matamshi hayo, hata hivyo amemtetea tena mwanawe wa pekee kuwa "jenerali mzuri sana" na kumpandisha cheo hicho siku chache baada ya mzozo huo kuzuka.
Akiwa afisa wa ngazi ya juu wa kijeshi, Kainerugaba anazuiwa kuzungumza hadharani kuhusu masuala ya kisiasa, lakini mara kwa mara amekuwa akiingia kwenye mijadala hiyo, na kusababisha mtafaruku wa kidiplomasia kwa Uganda.
Migogoro ya nchi za Magharibi
Ujumbe wake wa mtandao wa X kuwaunga mkono waasi wa Tigrayan nchini Ethiopia uliikasirisha Addis Ababa, huku mawazo yake kuhusu vita vya Urusi na Ukraine na mapinduzi ya 2021 nchini Guinea pia yaliibua sintofahamu.
Mwaka jana, alitangaza kwamba Uganda "itatuma wanajeshi kuilinda Moscow ikiwa itawahi kutishiwa na Mabeberu," akikemea mataifa ya Magharibi kwa kushiriki "propaganda zisizo na maana za kuiunga mkono Ukraine."
Mnamo mwaka wa 2013, polisi walifunga vituo viwili huru vya kuchapisha magazeti na vituo viwili vya redio kwa siku 10 baada ya kuchapisha mawasiliano ya siri yaliyovujishwa na jenerali mkuu akidai kuwa Museveni alikuwa akimuandaa Kainerugaba kumrithi.
Wengi wa washirika wa zamani wa Museveni, akiwemo daktari wake binafsi Kizza Besigye, wameachana na rais kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kupandishwa cheo kwa Kainerugaba, jambo ambalo pia limeibua hasira za wanasiasa wa upinzani na wakosoaji wa serikali.