Rais wa Nigeria Bola Tinubu ametaka uchunguzi ufanywe kufuatia ''ajali mbaya ya boti'' iliyoua takriban watu 150 katika jimbo la kati la Kwara.
Waliohusika katika ajali hiyo walikuwa wageni wa harusi. Walikuwa wakisafiri kurejea jimbo la Kwara kutoka jimbo jirani la Niger ajali ilipotokea Jumatatu usiku.
Shughuli za utafutaji na uokoaji zilikuwa zikiendelea, mamlaka ilisema. Chanzo cha ajali hiyo hakijafahamika mara moja.
"Nimesikitishwa sana na taarifa za ajali mbaya ya boti iliyogharimu maisha ya watu wetu katika Jimbo la Kwara"
"waathiriwa walikuwa wageni kwenye sherehe ya harusi na kufanya ajali hiyo mbaya kuwa chungu zaidi," rais Tinubu alisema katika taarifa iliyotolewa na ofisi yake ya vyombo vya habari siku ya Jumatano.
Kiongozi wa Nigeria alizitaka mamlaka katika jimbo la Kwara na mashirika husika ya shirikisho kuchunguza ''mazingira yanayozunguka ajali ya boti'' na pia ''kutatua na kuangazia sababu za ajali hii mbaya.''
Utekelezaji wa sheria
Huduma za dharura na wazamiaji wa eneo hilo wameendelea kutafuta watu kwani zaidi ya miili mia moja imepatikana hadi sasa.
''Kulingana na ripoti tuliyo nayo kwa sasa, takriban watu 150 tayari wamekufa na hiyo ni idadi kubwa sana,'' Ibrahim Umar Bologi, Amiri wa eneo la Pategi ambako wengi wa waathiriwa walitoka aliwaambia wanahabari Jumanne jioni.
Kiongozi huyo wa kimila alisema zaidi ya wengine 50 wameokolewa.
Rais Bola Ahmed Tinubu ametoa salamu zake za rambirambi kwa jamii na kuomba mashirika ya serikali kutoa msaada kwa manusura.
"Pole zangu za dhati na rambirambi kwa familia na marafiki wa waathiriwa wa ajali hiyo mbaya," Rais alisema.
Ajali za boti ni za kawaida nchini Nigeria mara nyingi husababishwa na mizigo kupita kiasi, utunzaji duni wa boti na hali mbaya ya hewa. Lakini ajali kubwa hivi ni nadra.
Rais Tinubu ambaye aliapishwa mwishoni mwa mwezi uliopita aliahidi kuwa utawala wake ''utaangalia changamoto za usafiri wa majini nchini ili kuhakikisha suala la usalama na viwango vya utendakazi vinazingatiwa kikamilifu''.