Akiwa amezaliwa miaka 44 iliyopita nchini Kenya, Nazizi ni chotara ambaye baba yake anatokea Kolkata nchini India wakati mama yake ni mzaliwa wa Mbozi mkoani Mbeya nchini Tanzania. 

Na Paula Odek

TRT Afrika, Istanbul, Uturuki

Nazizi Hirji, au Nazizi kama anavyojulikana kwenye ulimwengu wa Hip Hop na Dancehall Afrika Mashariki, si jina geni katika ulimwengu wa muziki katika ukanda huu.

Akiwa amezaliwa miaka 44 iliyopita nchini Kenya, Nazizi ni chotara ambaye baba yake anatokea Kolkata nchini India wakati mama yake ni mzaliwa wa Mbozi mkoani Mbeya nchini Tanzania.

Japo alifahamika zaidi na kundi la Necessary Noize akiwa na Wyre pamoja na Bamzigi, Nazizi aliingia kwenye tasnia ya muziki akiwa na miaka 16 tu, na kuachia ngoma ‘Ni sawa tu’, ambayo ilimtambulisha rasmi kwenye tasnia hiyo.

Japo alifahamika zaidi na kundi la Necessary Noize akiwa na Wyre pamoja na Bamzigi, Nazizi aliingia kwenye tasnia ya muziki akiwa na miaka 16 tu, na kuachia ngoma ‘Ni sawa tu’, ambayo ilimtambulisha rasmi kwenye tasnia hiyo./Picha: Nazizi

Nazizi alinukuliwa akisema kuwa alisukumwa kuingia kwenye tasnia ya muziki hasa baada ya kumuona baba yake akiandaa matamasha mbalimbali ya muziki na ndipo akaanza kuwasikiliza magwiji, kama vile Bob Marley na UB 40.

Ni shindano la kusaka vipaji la miaka ya 90 liitwalo ‘Da Show’ ambalo liliibua kipaji chake na miaka michache baadaye, akajiunga na akina Wyre na Bamzigi ndani ya Necessary Noize, ambapo kwa pamoja walifyatua vibao vikali vikiwemo ‘Kenyan Gal, Kenyan Boy’, ‘Bless My Room’, ‘Nataka Toa’ waliomshirikisha Nyota Ndogo, ‘Lovers Rock’, ‘Kama Sio Hii Muziki’ na vingine vingi vilivyoshika hisia za wapenzi wa Hip Hop na Rap Afrika Mashariki.

Mbali na kuwa sehemu ya Necessary Noize, Nazizi pia amewahi kujihusisha na kundi la East African Bashment Crew akiwa na mwenzake Wyre pamoja na Bebe Cool kutoka Uganda na kuachia vibao vikali kama vile ‘Fire Anthem’ na ‘Kube’.

Mbali na kuwa sehemu ya Necessary Noize, Nazizi pia amewahi kujihusisha na kundi la East African Bashment Crew akiwa na mwenzake Wyre pamoja na Bebe Cool./Picha: Nazizi

Ama kwa hakika, alifit sehemu zote iwe kwenye Hip Hop, Reggae au hata Dance Hall, na hili lilijidhihirisha baada ya kushirikishwa kwake na wasanii mbalimbali kama TID kutoka Tanzania katika, ‘Watasema Sana’ na wimbo ‘Raha’ ambaye alishirikishwa na Billnass na TID, wote kutoka Tanzania.

Pia amewahi kushirikishwa na msanii Prezzo kutoka Kenya katika wimbo ‘Let’s Get Down’.

Mwaka 2008, Nazizi alifunga ndoa na Mtanzania Vini Leopold ambaye walikuja kuachana miaka mitano baadaye.

Aliamua kupumzika kidogo masuala ya muziki baada ya kupata mtoto wake wa kwanza aitwaye Taafri Firoz, japo Christmas ya mwaka 2023 ilikuwa chungu kwa msanii huyo, baada ya kumpoteza mtoto wake wa pili Jazeel Adam, ambaye alifariki katika hoteli moja nchini Tanzania.

Nazizi aliweka ujumbe wenye hisia kwenye mitandao ya kijamii kuoneshwa kusikitishwa kwake na kumpoteza mtoto wake huyo, ambaye pia alikuwa na changamoto ya kusikia, akiwaomba mashabiki zake wampe faragha ili apate kuomboleza.

Nazizi aliweka ujumbe wenye hisia kwenye mitandao ya kijamii kuoneshwa kusikitishwa kwake na kumpoteza mtoto wake huyo, ambaye pia alikuwa na changamoto ya kusikia, akiwaomba mashabiki zake wampe faragha ili apate kuomboleza./Picha: Nazizi

Mwaka 2024, tuzo za Grammy zilimtambua Nazizi kama moja wa wanawake 10 wanaoheshimika katika tasnia ya Rap na Hip Hop barani Afrika.

Mbali na muziki, Naazizi ambaye ni binamu kwa Jaffar Nsham maarufu kama Jaffarai, msanii kutoka Tanzania ambaye alijulikana na wimbo wake ‘Niko Bize’, anapenda sana kujishughulisha na uanaharakati, akihamasisha masuala ya afya ya akili na uwezeshwaji wa wanawake.

Licha ya uchotara wake, Nazizi ameendelea kujisikia fahari ya asili yake, hususani alipoongeza urefu wa masikio yake na kutoboa pua yake mara mbili, akisisitiza kuwa ni ishara ya kuwaenzi mabibi zake.

Pia, amewahi kukaririwa akisema, maana ya jina lake kuwa ni ‘Binti wa Mzizi’.

TRT Afrika