Waziri Mkuu wa India Narendra Modi anajiandaa kuapishwa kwa ajili ya muhula wa tatu baada ya uchaguzi uliokuwa na ushindani mkali ambao matokeo yake yamekifanya chama chake kuunda serikali ya muungano.
Chama cha Modi cha Bharatiya Janata Party (BJP), ambacho kimekuwa madarakani kwa muongo mmoja kwa kupata ushindi mkubwa, kilikuwa kinatarajia ushindi ma kishindo.
Lakini matokeo ya uchaguzi wa wiki sita yaliyotolewa Jumanne yameonyesha chama cha BJP kikipoteza ushawishi wake na kukifanya kutafuta mshirika wa kuunda nae serikali.
Kundi la muungano lenye wajumbe 15 kutoka National Democratic Alliance (NDA) limetangaza siku ya Jumatano kwamba limekubali kuunda serikali.
"Sote kwa pamoja tumemchangua kiongozi anayeheshimika wa NDA Narendra Modi kuwa kiongozi wetu," kwa mujibu wa taarifa ya pamoja iliyotolewa na BJP.
Muungano huo una viti 293 bungeni, na kuufanya kuwa na ushawishi mkubwa katika bunge hilo lenye viti 543.
Taarifa ya vyombo vya habari nchini Indian inasema Modi ataapishwa kama waziri mkuu Jumamosi.
Wachambuzi wanasema Modi kutegemea muungano inamaanisha atakabiliwa na muhula wa tatu wenye changamoto.
"Itamlazimu Modi kuchukua maoni ya wengine — tutaona demokrasia zaidi na bunge lenye afya," amesema Nilanjan Mukhopadhyay, ambae ameandiika kitabu kuhusu maisha ya Modi.
"Atahitajika kuwa kiongozi ambae hakuwahi kuwa nae, tutamuona Modi mpya."