Mbunge wa Jimbo la Malava nchini Kenya, Moses Malulu Injendi amefariki dunia.
Mwanasiasa huyo alifariki Februari 17, 2025 katika hospitali moja jijini Nairobi nchini Kenya, kulingana na taarifa iliyotolewa na Spika wa Bunge la Kenya, Moses Wetang’ula.
Kwa mujibu wa Wetang’ula, Malulu alikuwa hospitalini hapo baada ya kuugua kwa muda mrefu, kabla ya umauti kumkuta.
Injendi alikuwa akihudumu kama mbunge katika muhula wake wa tatu, akiwa ameingia bungeni mwaka 2013.
"Alikuwa ni mwanasiasa aliyejitolea kuwawakilisha watu wake bila kuchoka tena kwa uadilifu mkubwa. Alifanya jitihada kubwa katika utungaji wa sera za sekta ya elimu pamoja na ile ya sukari ili kuboresha maisha ya wakenya, hakika tutamkumbuka," alisema Wetang'ula katika salamu zake za rambirambi.