Mshahara duni, mazingira mabovu ya kazi ni baadhi tu ya sababu zinawafanya madaktari kuondoka nchini Burundi na kwenda kutafuta ajira nchi nyengine. /Picha : TRT Afrika

Ramadhan Kibuga

TRT Afrika, Bujumbura, Burundi

Burundi inashuhudia wimbi kubwa la madakatari wake kuondoka nchini humo na kwenda kutafuta ajira katika nchi za kigeni. Hali hiyo imezorotesha huduma za afya katika baadhi ya hospitali za umma na kuwa kero kubwa kwa raia pale wanapohitaji kuonana hasa na madaktari bingwa kwa ajili ya tiba.

Mshahara duni, mazingira mabovu ya kazi ni baadhi tu ya sababu zinazowafanya madaktari kuondoka nchini Burundi na kwenda ugenini.

Kasi ya madaktari ya kuondoka nchini inatisha. Sio tu madaktari bingwa lakini pia wa madaktari wa kawaida.

Serikali ya Burundi kupitia wizara ya afya imekiri kwamba tatizo ni nzito na kutoa takwimu za awali: ''Madaktari zaidi 150 waliondoka nchini katika hospitali za umma 80. Na utoro huo ni katika kipindi cha miaka mitatu tu ya nyuma'' Alisema Waziri wa Afya Dkt Lidouine Baradahana, alipoalikwa bungeni kuzungumzia changamoto katika sekta ya Afya.

Inahofiwa kwamba pengine takwimu hizo ni ndogo ukilinganisha na hali halisi ''Ninachojua ni wengi wameondoka wanahudumu Rwanda, Kenya, DRC na Ufaransa ni mamia ya Madaktari'' Alisema Daktari na kuomba jina lake kuhifadhiwa

Na kuondoka huko kwa madaktari kunaacha uhaba mkubwa katika miundombinu ya afya. Na wagonjwa ndio wanateseka zaidi.

''Nilikwenda jana katika Hospitali ya Wilaya, lakini sikuonana na Daktari. Ndio maana nimeamua kuja hapa Bujumbura kutafuta daktari,'' mgonjwa Marie Nizigiyimana aliambia TRT Afrika. Mgonjwa huyu anatokea katika Wilaya Rutegama mkoa Muramvya kati kati mwa Burundi.

TRT Afrika ilitembelea pia Kliniki ya umma ya Rwagasore mjini kati Bujumbura na kukutana na kilio cha wagonjwa. ''Kama unavyoona nina matatizo ya macho, lakini tangu asubuhi nipo hapa kwa nia ya kuonana na Dkt wa macho , Lakini hatujampata. Na leo ni siku ya pili tunaambiwa tusubiri.Mpaka lini sasa?' Alisema Henry Misago huku akionesha kusosoneka.

Micheline yeye amemuona Daktari wake wa magonjwa ya wanawake lakini anaamini kuwa hali ni tete. ''Tunaiomba serikali kuimarisha maisha ya madaktari maana hatuna pa kukimbilia,'' aliambia TRT Afrika. ''Hatuna uwezo wa kwenda katika Hospitali binafsi kutafuta madaktari bingwa. Ugenini ndio usiseme. Tunakosa za kula, kweli tutapata za kujitunzisha nje?'' aliongeza.

Baada ya malalamiko hayo na uhaba mkubwa wa matabibu, madaktari wamevunja ukimya na kuelekeza lawama upande wa serikali ya Burundi.

Mwenyekiti wa chama cha madaktari (Synapses) alikiri kuwa ni dhahiri madaktari wanaondoka kwa wingi na kutaja kiini cha hali hiyo. "Kuna hospitali hazina tena madaktari . Sababu kubwa ni mshahara mdogo na kushindwa kukidhi mahitaji yao kutokana na gharama ya maisha kwa sasa''

Dkt Vincent Ndayizigamiye alilalamika kwamba kazi yao haithaminiwi vilivyo. ''Mshahara hauzingatii tena kwamba hii kazi ya daktari ni muhimu. Mshahara wa Daktari umesalia pale pale tangu mwaka wa 2019 karibu Franka laki 5, yaani Dollar 165 ndio maana unaona wengi wameondoka nchini na kwenda kufanya kazi ugenini. Wengine wamekwenda kwenye NGO's au katika hospitali za kibinafasi au kuachana kabisa na kazi ya udaktari,'' alisema.

Aidha Dkt Ndayizigamiye alisema madaktari walikuwa wamejenga matumaini makubwa katika sera mpya ya mshahara kwa wafanyakazi wa umma. Lakini matarajio yao yaligonga mwamba ''Saa za kazi za ziada na kazi za usiku hazikuzingatiwa. Hakuna marupurupu ya ziada, na hii imewavunja moyo madaktari wengi kusalia kwenye hospitali za umma. Hata Madaktari waliokwenda kupata ujuzi zaidi ugenini wamekataa kurudi nchini '' alisema Dkt Ndayizigamiye.

Wagonjwa hawana budi

Chama cha Madaktari wameonya kwamba uhaba wa madaktari utakuwa na athari kubwa na kuzorotesha afya ya raia.

''Sehemu ambako hamna Madaktari, raia hawapati matibabu ipasavyo. Kuna hofu ya kuongezeka visa vya maradhi hasa upande wa watoto na kinamama wajawazito ili hali Burundi ilikuwa imepiga hatua kubwa katika sekta hiyo''. Alisema Dkt Ndayizigamiye kwenye mazungumzo na vyombo vya habari. ''Hali hiyo itawalazimu raia kwenda kutafuta matibabu ugenini na katika hospitali za kibinafasi. Na hii ni ghali saana'' aliongeza.

Suluhu ya tatizo

Madaktari wameichagiza serikali kuchukua hatua za haraka.

"Kuna haja ya kuwastawisha kimaisha madaktari kwa kuongeza mshahara. Ndio njia pekee pia ya kuwahamasisha madakatari waliondoka nchini waweze kurejea Burundi, na kuleta vifaa vya kisasa ili kuweka mazingira mazuri ya kazi,'' alisema Dkt Ndayizigamiye.

Serikali inaamini Pia kuwa hali imeanza kutisha na tayari wameandaa mkakati wa kuwavutia tena madaktari.

''Serikali ya Burundi imeazimia kwanza kufikiria upya mkakati wa kuzuia madaktari wanaokwenda nje ya nchi,'' ilisema taarifa ya msemaji wa serikali Prosper Ntahorwamiye.

''Pili, kuhamasisha pia madaktari waelewe umuhimu wao wa kuwahudumia wagonjwa na raia. Tatu ,kufanya juhudi kuhakikisha huduma katika hospitali za umma zinatolewa kama vile wanavyohudumiwa wagonjwa katika hospitali za kibinafsi'' iliendelea kusema taarifa hiyo.

TRT Afrika