Katika mkutano wake Ijumaa, Ecowas ilitangaza vikosi vyake vya kijeshi viko tayari kuingilia kati mara tu amri itakapotolewa. / Picha: AFP

Mali na Burkina Faso zimetuma ndege za kivita nchini Niger ili kuonyesha uungaji mkono dhidi ya uwezekano wa kuingiliwa kijeshi na Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS).

Televisheni ya taifa ya Niger kwenye taarifa iliyopeperusha, iliangazia juhudi za pamoja za Mali na Burkina Faso kuunga mkono Niger na kutumwa kwa ndege za kivita ndani ya mipaka ya Niger siku ya Ijumaa.

"Mali na Burkina Faso ziligeuza ahadi zao kuwa hatua madhubuti kwa kutuma ndege za kivita kujibu shambulio lolote dhidi ya Niger," ilisema, ikieleza kuwa ndege hizo ni za kivita za Super Tucano.

Burkina Faso na Mali, zote zikiwa chini ya uongozi wa kijeshi, awali zilitoa taarifa ya mshikamano wao kwa Niger dhidi ya operesheni ya kijeshi iliyopangwa na ECOWAS kubadilisha mkondo wa mapinduzi nchini Niger.

Ilionya kuwa uingiliaji kati wowote utaonekana kama tangazo la vita dhidi ya Burkina Faso na Mali.

Jenerali Abdourahamane Tchiani, kamanda wa zamani wa walinzi wa rais wa Niger, alijitangaza kuwa mkuu wa serikali ya mpito mwezi uliopita, baada ya Rais Mohamed Bazoum kuondolewa madarakani katika mapinduzi ya kijeshi.

Wanamgambo wa kiraia

Kikosi cha wanamgambo wa kujitolea, ambacho kinajumuisha raia, pia kinapangwa nchini Niger ili kukabiliana na uingiliaji kati wa kijeshi wa ECOWAS.

Usajili wa kikosi cha wanamgambo cha kiraia unaoitwa Volunteers for the Defense of Niger (VDN) utaanza leo, Jumamosi katika mji mkuu, Niamey.

Watu wa kujitolea ambao wangependa kujiunga na VDN, wanatarajiwa kukusanyika katika Uwanja wa General Seyni Kountche ambapo yeyote aliye na umri zaidi ya miaka 18 anaweza kujiandikisha.

Juhudi kama hizo pia zimeanzishwa kwenye mipaka ya Nigeria na Benin.

Wanamgambo hao wataisaidia jeshi kupitia majukumu mbalimbali, zikiwemo za kupigana kwa silaha pamoja na huduma za matibabu, vifaa, msaada wa kiufundi na uhandisi pale itakapohitajika na utawala wa kijeshi.

Kundi kama hilo la wanamgambo wenye jina sawa lipo nchini Burkina Faso, huku wakitoa msaada kwa jeshi katika juhudi za kukabiliana na ugaidi.

TRT Afrika