Mali, Burkina Faso na Niger zimetangaza kujiondoa katika ECOWAS kutokana na uhusiano mbaya kati ya nchi hizo tatu na jumuiya ya kikanda ya Afrika Magharibi.
Katika taarifa ya pamoja siku ya Jumapili, Kapteni Ibrahim Traore wa Burkina Faso, Kanali Assimi Goita wa Mali, na Jenerali Abdourahamane Tchiani wa Niger walisema ni "uamuzi wao huru" kuondoka ECOWAS.
Waliongeza kuwa kuondoka kwao kutafanyika "bila kuchelewa."
Nchi hizo ambazo ziko chini ya utawala wa kijeshi kufuatia mapinduzi tofauti, zimeishutumu Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS) kwa kuzilenga isivyo haki, hasa kuhusiana na hali ya kisiasa na kiusalama katika mataifa hayo matatu.
Vikwazo
Niger, ambayo ilikuwa chini ya utawala wa kijeshi Agosti 2023 baada ya kuondolewa madarakani kwa Rais Mohamed Bazoum, inakabiliwa na vikwazo vya kiuchumi vilivyowekwa na ECOWAS, huku Burkina Faso ikishutumiwa kwa vitendo vya ukandamizaji, ikiwa ni pamoja na kukamatwa kwa vigogo wa kisiasa na mashirika ya kiraia.
Mali pia - mnamo 2022 - ilikabiliwa na vikwazo vya kiuchumi na kifedha baada ya watawala wa kijeshi kuchelewesha kurejea kwa utawala wa kiraia.
Wakati huo, Mali ilishutumu ECOWAS kwa "kunyonywa na mamlaka ya ziada ya kikanda kwa nia mbaya." Vikwazo hivyo viliondolewa baadaye, mnamo Julai 2022.
ECOWAS, yenye makao yake makuu katika mji mkuu wa Nigeria Abuja, kwa sasa ina nchi wanachama 15.
Nchi wanachama
Mataifa hayo ni Benin, Burkina Faso, Cape Verde, Cote d'Ivoire, Gambia, Ghana, Guinea, Guinea-Bissau, Liberia, Mali, Niger, Nigeria, Senegal, Sierra Leone, na Togo.
Lengo kuu la ECOWAS ni kukuza ushirikiano wa kiuchumi miongoni mwa nchi wanachama ili kuinua hali ya maisha na kukuza maendeleo ya kiuchumi.