Vyanzo vinne vya habari katika hospitali ya kijeshi vilisema takriban wanajeshi 50 waliojeruhiwa wameletwa hapo kwa matibabu./ Picha : Reuters 

Shambulio la mwishoni mwa juma lililofanywa na wanamgambo wa al Shabaab dhidi ya wanajeshi wa Somalia wanaoendesha mashambulizi dhidi yao liliacha makumi ya wanajeshi kujeruhiwa na idadi isiyojulikana kuuawa, wanajeshi waliohusika na maafisa wa hospitali walisema.

Uvamizi huo ulilenga wanajeshi katika mji wa Aus- wayne, ambao ulikuwa umetekwa kutoka kwa wanamgambo wenye mafungamano na al Qaeda siku zilizopita kama sehemu ya mashambulizi makubwa zaidi dhidi ya al Shabaab kuwahi kutokea kwa miaka kadhaa.

Kampeni za kijeshi katikati mwa nchi hiyo zilianza mwaka jana na zimeshika kasi katika siku za hivi karibuni, na kusababisha kutekwa kwa ngome ya wanamgambo wa El Buur siku ya Ijumaa.

Lakini shambulio la Aus-wayne Jumamosi lilionyesha udhaifu wa wanajeshi wa kukabiliana na mashambulizi katika maeneo ambayo al Shabaab wamejikita kwa muda mrefu.

Shirika la habari la Reuters linaripoti kuwa serikali ya Somalia imesema kwamba shambulio hilo lilizuiwa. Wasemaji wa kijeshi na waziri wa mambo ya ndani hawakujibu maombi ya maoni Jumatatu.

Vyanzo vinne vya habari katika hospitali ya kijeshi vilisema takriban wanajeshi 50 waliojeruhiwa wameletwa hapo kwa matibabu. Waliomba wasitajwe kwa sababu hawakuruhusiwa kuzungumza na vyombo vya habari.

Reuters