Raphael ni daktari wa mifugo wa kijijini ambaye mara kwa mara hutibu wanyama wa watu na kutoa ushauri kuhusu mifugo katika kijiji kidogo cha Kisaka huko Tanga, Tanzania. Anafanya biashara yenye mafanikio, na watu wanaaamini kazi yake, ambayo inaonekana kuwa na mafanikio.
Raphael hasa hutoa chanjo kwa ng'ombe kijijini, na dawa zake zinafanya kazi, na kwa hakika, biashara inanawiri kulingana na alivyosomea; kwa kweli, wakazi wa kijiji wanajua kuwa yeye ni mtu wa kuaminika na wanampelekea mifugo yao kwa ajili ya kupata matibabu.
Yuko vizuri na anajua kazi hiyo
Hata hivyo, kuna tatizo: Raphael ni tapeli, lakini wakazi wa kijijini kwake hawajui hilo; wanajua tu wanachokiona mbele yao kila siku wakati Raphael anafanya kazi na kutibu mifugo.
Imefichuliwa kuwa Raphael ni mhitimu wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine huko Morogoro na amekuwa akijaribu kupata kazi kwa miaka miwili sasa bila mafanikio. Akiwa na ujuzi na utaalamu alio nao, yeye ndiye mtu ambae ana utaalamu huo katika kijiji kizima. Lakini, hakuwa na idhini ya kufanya kazi hio, na sasa amekamatwa.
Hii na mifano mingine mingi ni sehemu ndogo tu ya tatizo kubwa zaidi linalohusiana na ukosefu wa ajira kwa vijana na umbali ambao mtu ataenda ili kujipatia riziki.
Takwimu zinasemaje?
Ingawa Afrika ina kiwango cha chini kabisa cha ukosefu wa ajira duniani kwa vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 24, asilimia 10.6 mnamo 2021, kulingana na Shirika la Kazi la Kimataifa, ILO, wengi wa vijana wa Kiafrika hufanya kazi kwa njia isiyo rasmi, na wengi wao sio kwamba wameajiriwa au wanaendelea kuishi katika umasikini licha ya kufanya kazi kutokana na mishahara duni na ukosefu wa akiba kwa ajili ya maisha ya mbeleni, hii inafanya iwe changamoto kulinganisha na nchi za Kiafrika na uchumi ulioendelea zaidi.
Mnamo 2024, karibu asilimia 11.2 ya vijana wa Kiafrika, wenye umri kati ya miaka 15 na 24, walitarajiwa kuwa hawana ajira. Kulingana na data kutoka ILO, takwimu hii haijabadilika sana tangu 2021.
Kuweka hili katika mtazamo unaoeleweka, zaidi ya moja ya vijana wanne barani Afrika - takriban milioni 72 - hawana ajira, na wawili kati ya watatu kati yao ni wanawake.
Afrika ina nafasi ya kipekee ya kuwa bara lenye vijana wengi na idadi ya vijana inayokua kwa kasi. Hii inaleta uwezekano mkubwa lakini pia changamoto mbalimbali.
Mambo yanayochangia
Matumaini ya ajira ya vijana wa Afrika yanapunguzwa na kiwango cha juu cha ukosefu wa ajira pamoja na ajira duni, pia kuna suala la viwango vya juu vya ongezeko la idadi ya watu, hasa kati ya kundi hilo la umri wa rika hilo.
Kuna tofauti katika ukosefu wa ajira kwa vijana kulingana na viwango vya elimu. Katika baadhi ya matukio, vijana walioelimika wanaweza kukabiliwa na changamoto za kupata kazi zinazoendana na sifa zao au kuwa na changamoto za fursa za kazi katika maeneo ya mijini.
"Kuna sera ambazo hazijawekwa kwa watu kuweza kujipatia riziki kutokana na mazingira ambayo hayafai kabisa hata kuanzisha biashara, hivyo hizi zinahitaji kutathminiwa upya katika sehemu nyingi sio tu za Tanzania lakini bara pia," anasema Fidelis Yunde, anayeendesha kituo cha Youth Movement for Change, YMC, asasi ya kiraia inalolenga kuleta maendeleo kwa vijana mkoani Singida, Tanzania.
Vijana wengi ambao wamepata elimu ya kutosha hupata changamoto kubwa mara tu wanapohitimu kutoka taasisi za elimu ya juu; wengine huchagua kuanzisha biashara wakati bado wanasoma ili kujipatia riziki.
Esther Pallangyo ni mwanafunzi aliyesomea Chuo Kikuu huko Morogoro, Tanzania, kama mwanafunzi wa maendeleo ya vijijini. "kuna kasoro katika mfumo ambapo wanafunzi wengi wanahitimu, lakini hakuna kazi za kutosha." Esther anaiambia TRT Afrika. Mkazi huyo wa Mwanza sasa amerudi nyumbani na amekuwa akisubiri kazi kwa zaidi ya miaka miwili.
Mbinu Zinazolenga Suluhisho
Serikali za Afrika na washirika wa maendeleo wamejaribu kukabiliana na changamoto ya ajira kwa kutekeleza programu za maendeleo ya ujuzi kwa ajira katika sekta zenye kipaumbele kama kilimo na uzalishaji, na kukuza ujasiriamali.
Fidelis anapendekeza mafunzo ya kuwaongeza ujuzi kwa vijana ambao wana hitimu na kutafuta kazi ili kuonekana wanafaa zaidi kupata kazi kama wanavyofanya kwa shirika lao mara kwa mara. Tatizo jingine, anasema, ni kwamba vijana mara nyingi hawajitangazi vyema, ambayo ingeongeza nafasi zao za kupata kazi.
Vijana waliojiandikisha katika programu kama hizo hujifunza ujuzi wa kiufundi na ufundi na ujuzi mwingine wa maisha kuwasaidia kupata ajira na kuendesha biashara zao wenyewe.
"Watu mara nyingi wanaogopa kuanzisha biashara pia. Fikiria mimi kuweka hela zangu kidogo za kubangaiza kwenye biashara, na sifanikiwi, sio rahisi." Anasisitiza mhitimu Esther kuhusu kujitosa katika ujasiriamali.
Mifano barani
Violet Ayubu ni Mkurugenzi wa Vision for Youth, shirika lisilo la kiserikali linalofanya kazi ya maendeleo kwa vijana iliyoko Arusha, Tanzania. Anafafanua baadhi ya njia na mifano kutoka kote Afrika ambayo inawapa vijana katika bara hilo nafasi kidogo zaidi katika mazingira waliopo.
"Kenya wako na baraza la vijana ambalo lina miradi maalum kwa ajili ya vijana. Ulaya wao wanatuma vijana kufanya kazi za kujitolea kwa mwaka wa mapumziko na inawapa uzoefu. Kuna BBT, Building Better Tomorrow, (Tanzania) lakini bado haijafikia vijana wengi. Iko chini ya wizara ya kilimo." aeleza Violet na kusisitiza kuwa ongezeko la ukosefu wa ajira inakadiriwa kuongezeka kila mwaka kwa takribani asilimia tatu wakati kwa sasa ukosefu wa ajira ni asilimia 80 ikiwa wengi ambao hawana kazi ni vijana.
Wazazi wengi wa Kiafrika wanakatisha tamaa watoto wao kujiingiza katika kazi za ubunifu kama uandishi, sanaa, na muziki, wakiona zaidi kama jambo la kupitishia muda yani hobby. Hata waandishi maarufu wa Kiafrika kama Chinua Achebe na Chimamanda Ngozi Adichie kutoka Nigeria walisomea udaktari kutokana na msukumo wa wazazi.
Kuwawezesha vijana kwa maarifa yasiyo na mipaka ni muhimu kufikia maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi na kupunguza hatari za kukutana na visa kama vile vya daktari feki kama Raphael.