Alex John mkazi wa Dar es Salaam kutoka Mkoa wa Mbeya, Tanzania. Picha/TRT Afrika.

Na Juma Issihaka

TRT Afrika, Dar es Salaam, Tanzania

Wingi wa watu, fursa na huduma ni miongoni mwa sababu zinazowafanya vijana wengi nchini Tanzania, na maeneo mengine kufungasha virago kutoka vijijini na kwenda kuanza maisha katika maeneo ya mijini.

Wengi wanaamini kuwa, ni rahisi kufanikiwa mjini kwa sababu kuna fursa nyingi za ajira, tofauti na ilivyo vijijini.

Lakini baada ya kujitosa katika maisha ya mjini, baadhi wamejikuta wakitamani kurudi kijijini kwa kile wanachokieleza kuwa, maisha ya mjini ni magumu kuliko walivyotarajia.

Utafiti

Utafiti uliofanywa na Taasisi ya Tafiti za Kiuchumi (Repoa) mwaka 2021, unasema kiwango cha watu wanaohama kutoka vijijini kwenda mijini nchini Tanzania kimefikia wastani wa asilimia 15.

Kulingana na utafiti huo, wenye kichwa cha habari 'Mageuzi ya Miji nchini Tanzania' inakadiriwa kwamba, kufikia mwaka 2030 idadi ya watu katika miji nchini humo, itaongezeka na kufikia 35.5 milioni.

Ongezeko limekadiriwa zaidi kufikia mwaka 2050, ambapo miji ya Tanzania itakuwa na jumla ya watu 76.5 milioni.

Utafiti huo uliofanywa kwa kushirikiana na Taasisi ya Friedrich Ebert Stiftung (FES), unakadiria pia kwamba, watu katika Jiji la Dar es Salaam wataongezeka na kufikia milioni 10, wakati Sensa ya watu na Makazi ya mwaka 2022 imebainisha uwepo wa watu 7.4 milioni katika jiji hilo.

Haukuishia hapo, utafiti huo uliofanywa katika Mikoa ya Njombe, Arusha na Dar es Salaam, unabainisha asilimia 38 ya wakazi wa mikoa hiyo wamehama katika maeneo walikozaliwa.

Kati ya hao waliohama, asilimia 58 wamehamia katika Jiji la Dar es Salaam, huku kundi la vijana wenye umri kati ya miaka 15-35 likiwa kubwa zaidi ya wenye umri wa miaka 35-55 na hakuna mwenye umri zaidi ya hapo.

Luca Isaya, mkazi wa Dar es Salaam kutoka Kilimanjaro nchini Tanzania. Picha/TRT Afrika.

Ugumu wa maisha

Ugumu wa maisha ya vijijini ndiyo unaochagiza vijana wengi kuhamia mjini, wakidhani kuna maisha bora na rahisi, kama inavyoelezwa na Luca Isaya, mzaliwa wa Mkoa wa Kilimanjaro nchini Tanzania.

"Kijijini kazi zinakosekana, kwa mfano, zingekuwa zinapatikana hata mimi mwenyewe nisingekuja huku (mjini). Ningekuwa na mtaji wa kulima ningebaki huko huko kijijini."

Luca Isaya, mkazi wa Dar es Salaam

Luca alihama kijijini mwake mwaka 2012 na sasa sehemu kubwa ya maisha yake ni jijini Dar es Salaam, eneo ambalo ndilo msingi wa kipato chake kutokana na shughuli zake za ulinzi.

Kwa mujibu wa kijana huyo wa kimaasai, kilichomshinda kijijini ni ugumu wa maisha na uchache wa fursa za kazi, hivyo hakuona namna nyingine tofauti na kwenda Dar es Salaam.

"Kijijini kazi zinakosekana, kwa mfano, zingekuwa zinapatikana hata mimi mwenyewe nisingekuja huku (mjini). Ningekuwa na mtaji wa kulima ningebaki huko huko kijijini," anaeleza.

Glory Mrema kutoka Manyara, Tanzania. Picha/TRT Afrika. 

"Kazi ninayofanya (Dar es Salaam) ni ulinzi na kijijini nilikuwa mfugaji, nina mifugo kidogo sio mingi, nimeacha inahudumiwa na wadogo wangu," anasema Luca.

Uamuzi wake wa kutafuta fedha mjini, anasema umekuwa shubiri kwa nyakati fulani, kwani familia yake inaamini ana kipato kikubwa tofauti na anachowatumia.

Hata hivyo, anasema aliyokutana nayo mjini ni tofauti na alivyotarajia, kila kitu kinahitaji fedha ikiwemo malazi, chakula na hata maji ya kunywa na huduma nyingine, ambazo kijijini zingepatikana bure.

"Ugumu wa mjini ni hela tu hazipatikani mara kwa mara. Unataka uwe na hela za kula, za kulipia sehemu za kulala na za kutuma nyumbani ndiyo zinakuwa changamoto.

Kijijini tukihamisha ng'ombe porini tunakwenda kuchunga, kwa hiyo haulipii chochote," anasema.

Wingi wa fursa

Mbali na Luca, Glory Mrema mzaliwa wa Mkoa wa Manyara Kaskazini mwa Tanzania amejikuta amezamia jijini humo tangu mwaka 2014 alipoingia kwa ajili ya masomo ya elimu ya juu.

Anasema tangu alipohitimu elimu hiyo mwaka 2016, hakuona sababu ya kurudi kijijini kwa kuwa kuna shughuli anazofanya zinazomuingizia kipato, ambazo asingezifanya iwapo angelikuwa kijijini.

Kulingana na Glory, alipokuwa chuoni, alianza biashara ya kuuza nguo mtandaoni, shughuli ambayo imemfanya asitamani tena kurudi kijijini, licha ya kwamba amekosa ajira ya taaluma aliyosomea.

"Nilisoma Uhifadhi wa Nyaraka (Records) sijapata ajira lakini nimejiajiri katika biashara ya nguo mtandaoni. Sioni haja ya kurudi kijijini kwa sababu huku ninaingiza chochote.

Mara nyingi wananchi huamia mijini wakitafuta kazi za uchuuzi kuendesha maisha yao. Picha/TRT Afrika.

Kama si shughuli hii, muda huu ningekuwa kijijini nafanya shughuli za kilimo ambacho si cha uhakika," anasema.

Kinachomfanya Glory aendelee kubaki jijini Dar es Salaam, ni kile anachokiita uwepo wa mzunguko wa fedha ambao ni nadra kuwepo kijijini.

Anaeleza hata biashara yake ya kuuza nguo mtandaoni, isingefanikiwa iwapo angelikuwa kijijini kwa sababu inahitaji uwepo wa mtandao 'internet' ambayo kijijini kwao haipo.

Lakini shughuli za kilimo ambayo ndio tegemezi kubwa kwa watu wa vijijini, ni moja wapo ya vitu vilivyomfanya Glory ayakimbie maisha hayo na kuendelea kusalia Dar es Salaam huku akisema kuwa licha ya kilimo kutokuwa na uhakika lakini pia kinachosha.

Tofauti na Luca, Glory anasema safari yake ya mjini imekuwa na mafanikio kwa sababu Dar es Salaam kuna idadi kubwa ya wateja wa bidhaa zake, hivyo inamwezesha kufanya biashara na kujikimu kimaisha.

"Mimi sijutii kuja mjini. Kwanza nilikuja kusoma, ajira sijapata nimejiajiri nafanya biashara zangu. Hii ni nzuri kwangu, nalisha familia," anasema.

'Msoto Mjini'

Alex John aliyetokea Mkoa wa Mbeya uliopo Kusini Magharibi mwa Tanzania ambae kwa sasa yuko Dar es Salaam, anasema si rahisi kuishi mjini kama wengi wanavyodhani, akifafanua kuwa kuna msoto mkali.

"Siwezi kutamani kurudi kijijini kwa sababu nikisema narudi kijijini, naenda kuanza upya. Anayetamani kuja mjini, aje kwa sababu huku biashara yoyote unayofanya na kuna mkusanyiko wa watu."

Said Sued, mkazi wa Dar es Salaam

Anasema alifika Dar es Salaam mwaka 2016 baada ya wazazi wake kufariki, akidhani kufika mjini ndio itakuwa mwisho wa matatizo yake.

"Unakuta hata marafiki tuliowaacha kule huwa wananipigia simu kwamba niwarushie buku (Sh1,000). Yaani wanahisi ukishafika mazingira ya Dar es Salaam, mshikaji katoboa (kafanikiwa).

Hawajui kama huku kwenyewe kuna msoto mkali," anasisitiza.

Magumu aliyokutana nayo katika jiji hilo, anasema yamemfanya atamani kurudi nyumbani kwao (Mbeya), lakini kwanza anatafuta fedha zitakazomwezesha kufanikisha hilo.

"Nilikuwa nafiriki nikifika Dar es Salaam, maisha yanaweza kidogo kuwa afadhali, lakini nilipofika hapa (mjini Dar es Salaam), tofauti na kile nilichokitarajia, maisha yamenichapa," anasema Alex.

Sitamani kurudi kijijini

Mambo ni tofauti kwa Said Sued aliyetokea Mkoa wa Kagera, uliopo Kaskazini-Magharibi mwa Tanzania, anayesema hatamani kurudi kijijini kwa kuwa atakwenda kuanza upya.

"Siwezi kutamani kurudi kijijini kwa sababu nikisema narudi kijijini, naenda kuanza upya. Anayetamani kuja mjini, aje kwa sababu huku biashara yoyote unayofanya na kuna mkusanyiko wa watu," anasema.

Said anasema safari yake kutoka kijijini kwenda mjini mwaka 2011, ilitokana na wito wa mmoja wa watu aliyekuwa anafahamiana naye, aliyemtaka aende mjini kwa ajili ya shughuli mbalimbali.

"Akaniambia njoo Dar es Salaam tumekutafutia kazi, kwa hiyo nikafika. Nikipouliza nafanya kazi gani, akanambia kwani huzioni? Nikaambiwa usiku tumekula umeona vyombo vichafu na mama atakupa nguo chafu ndiyo kazi zenyewe hizo.

Niliamua nitulie siwezi kusema nikimbie nirudi Bukoba, moja kwa moja nikawa nimejua kazi nilizoitiwa ni za ndani," anasema.

Anasema ameifanya kazi hiyo kwa miaka miwili na baadaye aliuhama kutafuta shughuli nyingine na ndipo alipojikuta katika Soko la Shekilango akifanya biashara ya mbogamboga.

Hatari vijana kukimbilia mjini

Mchambuzi wa Masuala ya kijamii kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Faraja Kristomus anasema vijana wanahitajika vijijini ili waendeleze uchumi wa maeneo hayo.

"Tusipokuwa makini, vijana wengi wakihamia mjini, nguvu kazi ya vijijini itapotea, tutabaki na kundi kubwa la wazee. Shughuli za uchumi zitadorora kama kilimo, ufugaji na nyingine," anasema.

Vijana wanaona mijini kuna fursa kutokana na mzunguko wa pesa lakini pia idadi kubwa ya watu wenye mahitaji tofauti. Picha/TRT Afrika. 

Wanafuata faida

Anasema vijana wengi hufanya uamuzi wa kwenda mijini kutokana na kukosa faida ya kile wanachokizalisha vijijini.

"Wanadhani mijini ni rahisi kutengeneza fedha na faida. Bahati mbaya, wanapofika mijini wanakutana na mazingira tofauti na kile walichoaminishwa walipokuwa kijijini," anasema.

Anasema kinachowafanya wengi waamini mjini kuna fedha ni namna wenzao waliokwenda huko wanavyoonekana wamependeza na kunawiri.

Mambo ya kuzingatia

Kabla ya kuamua kwenda mjini, Dk Faraja anasema muhimu kujua nini utakwenda kufanya.

"Wale vijana wenye karama ya biashara, ujuzi mbalimbali mjini ni rahisi kupata kazi kwa sababu mtaji mkubwa wa mjini ni wingi wa watu na biashara inayokuwa na watu wengi huingiza faida," anasema.

Wito kwa Serikali

Anasisitiza ili kuvutia vijana wengi vijijini, ni vyema serikali za nchi za Afrika, ziongeze tija kwenye shughuli wanazozifanya katika maeneo hayo, ikiwemo kilimo. Anasema ni vema vijana wa kijijini wakafundishwa mbinu mbalimbali za matumizi ya fedha, teknolojia na kuwepo miundombinu itakayowafanya wabaki vijijini.

"Uwepo wa barabara, umeme, maji, mawasiliano, na vitu kama hivyo, vinaweza kuwafanya vijana wakashawishika kubaki vijijini kwa sababu wengi wanapoteza ndoto zao kwa kuja mijini," anasema.

Anasema anayetamani kwenda mjini ni vyema akawa na ujuzi wa kumuingizia kipato na ajue atakwenda kufanya nini, vinginevyo atakutana na makundi ya watu wasio salama na kuharibu ndoto zake.

TRT Afrika