Ronald Sonyo
TRT Afrika, Dodoma, Tanzania
Ni majira ya jioni, Dina Simbangui, mama wa watoto watatu akiendelea na maandalizi ya chakula cha jioni. Moshi unafuka jikoni, huku akiendelea kuukoleza kwa kutumia mikono yake ambayo haina vidole. Ni athari zitokanazo na ugonjwa wa ukoma, baada ya kuuguwa kwa miongo kadhaa.
Dina, ni sehemu ya wakazi 62 wa kitongoji cha Samaria kilichopo Mkoani Dodoma nchini Tanzania.
Kijiji hichi awali, kilitengwa na serikali kama sehemu maalumu ya kupokea na kutoa matibabu kwa wale waliopatwa na ugonjwa huo, ambao katika miaka ya 70 mpaka 80 ulisumbua nchi nyingi duniani, ikiwemo bara la Afrika.
Ni ugonjwa ambao, uliambatana na unyanyapaa kwa kiasi kikubwa, huku wengi wakiuhusisha na ushirikina. Wataalamu wa afya wanakiri kwamba, hii yote ilichangiwa na uwelewa mdogo miongoni mwa jamii.
Hivi sasa, matumizi ya kijiji hicho yamebadilishwa, na kufanywa makazi ya kudumu kwa waliosalia kuwa waathirika wa ugonjwa huo.
Hichi ndicho chanzo cha Dina Simbangui na mume wake Saimon Mkoi kujikuta kijijini hapo. Wameishi miaka mingi lakini simulizi zao zinatofautiana.
Saimon Mkoi, yeye alizaliwa mwaka 1942 wilayani Kilosa Mkoani Morogoro, lakini maisha yake yalibadilika mwaka 1962 baada ya kuugua ukoma.
Anakumbuka enzi za ujana wake kabla ya kuumwa, alipokuwa mkulima wa mazao mbalimbali kama vile mahindi na maharagwe.
“Mimi nilikuwa kijana safi kabisa, lakini nilipokaribia miaka 30 ndipo nilipoanza kuumwa. Nilikuwa Kilosa na nilikuwa mkulima lakini sasa nashindwa kulima na mikono haina kazi,” anasimulia.
Katika kusaka matibabu, alifika katika hospitali kadhaa ikiwemo Turiani, Sukamahela na ifakara, zote zipo mkoani Morogoro. Harakati hizi hazikuzaa matunda. Kwa sababu mfa maji haachi kutapatapa, hatimae, alijikuta katika kijiji cha Samaria.
“Kote nilitembea kwa sababu ya kupata matibabu, lakini nilipofika Hospitali ya kilosa sikuwa na habari kama naumwa ukoma, lakini nilieleweshwa kwamba tayari nilikuwa na ukoma,” anaiambia TRT.
Nae Simbangui, mke wa Mkoi, yeye alizaliwa Wilayani Mpwapwa Mkoani Dodoma na tangu alipofika kijijini hapo, anasema, katu hajatembelewa na ndugu zake, walioamua kumtenga kabisa.
“Wataalamu walipogundua kuwa naumwa, na sina msaada wowote kutoka kwa ndugu, ndipo nilipoamua kuja kukaa hapa kwa ajili ya kupata matibabu ya karibu. Na huo ndio ulikuwa mwanzo wa mimi kuishi hapa. Mpaka sasa, hakuna ndugu aliye kunitembelea” anasimulia.
Mbali na wahisani kuwajengea makazi ya kudumu, lakini baadhi wameiambia TRT Afrika kwamba kwa sasa wanachokosa ni huduma za matibabu ya bure, pamoja na mahitaji muhimu kama vile chakula na malazi.
“Ukienda Hospitali unakaribishwa vizuri lakini wakishakutibu wanakudai malipo, wanasema hii Hospitali haipo kwa ajili yetu pekee. Sisi ni walemavu tunaotegemea Serikali, lakini nayo imetutupa,” anasema.
Ingawa hivi sasa wamepona ugonjwa wa ukoma lakini athari za ugonjwa huo bado zipo mwilini. Mara kwa mara wanapatwa na magonjwa nyemelezi kama kutokwa na vidonda.
Kwa upande wake, Mary Manyono ambaye ni muangalizi Mkuu wa wazee hao, alikiri kuwepo kwa chagamoto.
"Njaa ipo na wanahangaika sana, hakuna vyoo, hakuna umeme, wala mashine za kusaga na kwenda kijijini kusaga ni mbali? anasema Mary.
Serikali imesema kiwango cha ukoma kimeshuka kutoka wagonjwa 2,297 mwaka 2015 hadi wagonjwa 1,309 mwaka 2023 sawa na punguzo la 57%.
Takwimu zinaonesha hadi kufikia mwaka 2023, Tanzania ilikuwa na wagonjwa 3 kwa kila watu 100,000 hivyo kufikia kiwango cha awali cha Shirika la Afya Duniani (WHO) kutokomeza ukoma.
Hata hivyo, Serikali imetoa wito kwa halmashauri 19 katika mikoa tisa ya nchi ukiwemo Dodoma, kuwaibua wagonjwa wa ukoma,kufuatilia mwenendo wa ugonjwa, na kuweka takwimu sahihi. Dodoma ni miongoni mwa mikoa ambayo haijafikia viwango vya kutokomeza ugonjwa huo.
“Bado kuna halmashauri 19 katika mikoa ya Morogoro, Lindi, Dar es Salaam, Mtwara, Kigoma, Tanga, Dodoma, Geita, na Pwani ambayo haijafikia viwango vya utokomezaji,” ilisema taarifa hiyo.
Pamoja na kutoweka kwa ukoma, imekuwa ni utamaduni wa kila mwaka kuadhimisha siku ya Ukoma duniani, lengo ikiwa ni kufanya tathmini na kuangalia baadhi ya changamoto zilizopo.