Na Mwandishi Wetu
TRT Afrika, Morogoro, Tanzania
Ni ngoma iliyojizolea umaarifu mkubwa katika siku za hivi karibuni nchini Tanzania, hasa baada ya video zake kusambaa kwa wingi kwenye mitandao ya kijamii ikiwemo ule wa ‘tiktok.’
Ngoma hii huchezwa wakati wote wa mwaka lakini zadi, katika kipindi cha kiangazi baada ya mavuno pindi watu wanapojiandaa na msimu mpya wa kilimo na sherehe za mwisho wa mwaka. Japokuwa huchezwa katika matukio ya furaha na hata ya huzuni kama vile harusi na wakati wa kumaliza misiba. Kinachobadilika ni aina tu ya nyimbo kati ya tukio moja hadi jengine.
Ngoma hii iliitwa Chunda ikimaanisha pale uliposimama, ni neno la kabila la Kiluguru na hii inatokana na wachezaji kusimama eneo moja tu kwa kipindi chote watakachokua wanacheza mpaka pale watakapokua wamekamilisha shughuli eneo husika hata ikitokea wamepumzika basi wakirudi husimama eneo lilelile na kuendelea kucheza.
Zaidi, ngoma hii huchezwa na wanaume hasa vijana kutokana na matumizi makubwa ya nguvu wakati wa kucheza lakini pia, kwa mujibu wa mzee Rajab Almasi, ambaye ni kiongozi wa kikundi cha Twariq Kadiria, anasema mara nyingi wanacheza wanaume ili kuepusha mihemuko ya kihisia baina yao na wanawake.
“Tunacheza watoto wakiume kutokana na tunamtaja Mungu zaidi, hakuna kilevi kinachotumika pale. Unajua tunapochanganyika na watoto wa kike huwa tunahisia tofauti.’’
Ngoma hii huchezwa na vijana wa rika zote kuanzia miaka 18. Jambo linaloipa mvuto wa kipekee na kinachoifanya ipendwe zaidi kwa sasa ni miondoko yake ya uchezaji, kwani ni ngoma bila ngoma, bali upigaji wa miguu chini kwa pamoja na sauti kali nzito za waimbaji hutengeneza mtiririko wa kuvutia wa sauti.
Uchezaji wake huwa kwa mfumo wa duara lakini huwa na duara zaidi ya moja kutokana na wingi wa wachezaji na muimbaji mkuu huwa katika duara dogo ya ndani ijapokua mara kadhaa wanachoimba dura la ndani hutofautiana na wanachoimba dura la nje lakini uchezaji wao wote hufanana na zaidi duara ya nje hutawaliwa na vijana zaidi huku duara ndogo la ndani lichukuliwa na watu wa umri wa makamo na wazee.
Chedieli Senzige ni mwalimu wa sanaa aliyehitimu kwenye Chuo cha Sanaa Bagamoyo- Tasuba na kwa sasa anafanya shughuli zake za kisanii na ufundishaji wa saana mkoani Morogoro, anasema ngoma hii ya Chunda ni mafanikio ya utamaduni, “Hii ngoma ya chunda sio ngoma ya jadi kwa asilimia 100 bali mchanganyiko wa usasa na utamaduni.”
"Vyote hivyo huonekana kwa pamoja kwenye mpangilio wa sauti, uchezaji lakini pia mavazi, kwani imezoeleka ngoma ya asili lazima wachezaji wawe na mavazi maalumu ya kitamaduni wakati wakuicheza ambayo huwatambulisha, lakini pia baadhi huwa na vifaa au ala, lakini kwa ngoma hii kila mtu huvaa nguo yake yoyote kuanzia juu mpaka chini hakuna sare yoyote zaidi ya kwenye hatua za uchezaji," anasema.
Mkoa wa Morogoro almaarufu kama “Mji kasoro bahari” una ngoma nyingine kama vile Mangaka na Ngokwa ambazo nazo huchezwa wakati wa matukio mbalimbali ya mkoani humo ambapo kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi mwaka 2022 una jumla ya wakazi 3,197,104 wanaume 1,579,869 na wanawake 1617,235huku shughuli zao kubwa za kiuchumi zikiwa ni kilimo na ufugaji.
Mbali na ngoma hizo kutoka Mkoa wa Morogoro, Tanzania pia inajivunia kuwa na makabila zaidi ya 100 ambayo yote yana tamaduni tofauti.