Masoud Sumuni akimhudumia mmoja wa wagonjwa nyumbani kwake Zuzu, Dodoma, Tanzania. Picha/TRT Afrika. 

Ronald Sonyo

TRT Afrika, Dodoma, Tanzania

Kama wewe ni mtumiaji wa mitandao ya kijamii, bila shaka jina la Masood Sumuni, ambae ni mganga wa tiba asili litakuwa sio geni masikioni mwako.

Umaarufu wa Sumuni, mkazi wa kijiji cha Zuzu, kilichopo nje ya jiji la Dodoma, umezidi kukuwa kutokana na mtindo wake wa kutibu wagonjwa wenye matatizo ya mifupa na majeraha bila kugusa eneo lenye tatizo.

Mzee Sumuni ni nani?

Ana umri wa miaka 77 kutoka jamii ya wafugaji kule Mkoani Shinyanga.

Utaalamu wa kutibu aliurithi kutoka kwa baba yake mzazi ambaye alikuwa mtaalamu wa tiba asili huko Tabora.

“Siku moja, ng'ombe alivunjika mguu, baba akaleta dawa na kuniambia niitengeze, tukaiunguza ile dawa mpaka ikawa kama mkaa. Hapo tukaanza kumtibu ng’ombe kwa kuchanganya na mafuta na baadaye ngo’mbe alianza kutembea,” anasimulia.

“Nilipohamia Dodoma, mwaka 1977, mtoto wa jirani alivunjika mkono na nikatengeza dawa na kumtibu na hatimae akapona. Hapo nikajua kwamba natakiwa kuanza kutoa tiba asili,” anaongeza.

Tangu wakati huo, umaarufu wake umefika mbali na kuvutia wateja kutoka maeneo mbalimbali ya nchi ikiwemo Dar es Salaam, Dodoma, Morogoro na kuendelea. Mbali na kutoa tiba, lakini pia, fani hiyo imekuwa njia ya kujipatia kipato cha kila siku. Mgonjwa mmoja analipa ada ya shiling elfu 8 ambazo ni sawa na dola 3 za Kimarekani.

Kawaida mgonjwa analipishwa kiasi cha shilingi efu 8 kwa ajili ya matibabu. Picha/TRT Afrika. 

Mtindo wake wa kuunganisha mifupa iliyovunjika bila kugusa hata yeye mwenye unamshangaza. Anasema kuwa hakuwahi kujua kwa nini baba yake alikuwa akifanya hivyo, zaidi ya yeye kufuata nyayo za baba yake.

“Utaratibu huu ulikuwa wa baba, na sikuweza kumuuliza kwa nini anafanya hivyo. Nilikuwa namuona akishika mguu na kuukanda kwa maji ya moto, lakini dawa haikuwa inagusa jeraha,” anasema.

Masood alisema anafurahia kazi yake na jinsi anavyotibu wagonjwa bila kupata malalamiko ya dawa zake kutokufanya kazi.

“Wagonjwa wengi ni vijana na watoto pengine hii ni kutokana na ajali za pikipiki,” alisema huku akisisitiza kwamba, ameanza kurithisha familia yake kutoa matibabu hayo.

Matibabu yanayofanyika, yanaweza kuchukua wiki moja hadi mbili mpaka kukamilika. Picha/TRT Afrika. 

Je, ni suala la matibabu au imani?

Nyumbani kwa mzee Masoud, miongoni mwa wanaoendelea kutibiwa ni Shabani Hamud, dereva wa pikipiki maarufu Boda, yeye anasema baada ya kupata ajali na kuvunjika mkono, ameanza kupata matumaini baada ya kupata matibabu kutoka kwa Masood.

“Kila kitu ni imani, na imani yangu ndio imenileta hapa. Wapo ninaowafahamu waliopona na mimi nitakamilisha matibabu baada ya wiki mbili. Mungu akipenda nitapona,” anasema huku akionyesha matumaini.

Mzee Masoud anasema hamu yake ni kuboresha makazi yake ili kutoa malazi kwa baadhi ya wagonjwa. Picha/TRT Afrika. 

"Aina hii ya tiba kweli ni mpya kwangu na sikuwahi kuiona kabla. Sisi tumezoea kuona watu wakifungwa mbao, lakini kwa kweli haya kwangu ni maajabu?" anasema.

Fikiri Aloyce, ametoka jijini Dar es Salaam mpaka katika kijiji cha Zuzu kupata matibabu baada ya madaktari kupendekeza mkono wake ukatwe.

“Unapokuwa na matatizo matumaini huwa madogo lakini mimi nimepona. Kwa sasa, naweza kuendesha pikipiki, kupika na hata kubeba ndoo ya maji lita 20. Kweli siamini kama naweza kufanya shughuli zangu za kila siku,” alisema.

Tiba asili nchini Tanzania, inatambuliwa rasmi. Hata hivyo, serikali imeweka utaratibu maalumu ambao lazima ufuatwe ikiwemo kusajiliwa ili kutambulika rasmi.

Kulingana na Dk Simon George Chiteto ambaye ni msimamizi wa huduma ya tiba asili katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, wataalamu wa afya pamoja na Wizara ya Afya inazitambua tiba asili.

Amesema mara nyingi kabla ya tiba hizo kutumika kwa wagonjwa hupitia kwenye michakato kadhaa ikiwemo utafiti ili kujiridhisha kwamba hazina madhara yeyote kwa kufuata viwango vilivyopendekezwa.

"Tiba za asili ni kitu kinachotambulika na kwa kweli, tunakitumia na tunawaandikia wagonjwa wetu na wanapona," alisema na wakati huo huo kuongeza, "Jambo la msingi ni tiba hizi zipitishwe na wataalamu wa afya," ameongeza.

TRT Afrika