Kundi la waasi lenye uhusiano na Al-Qaeda siku ya Jumanne lilidai kuhusika na shambulio kwenye uwanja wa ndege wa kijeshi na kituo cha mafunzo huko Bamako, likiwa ni shambulio la kwanza la aina yake katika miaka mingi kuukumba mji mkuu wa Mali.
Kundi la JNIM lilisema kwenye kupitia vyombo vyake vya mawasiliano kwamba "operesheni maalum" ililenga "uwanja wa ndege wa kijeshi na kituo cha mafunzo cha askari wa kijeshi wa Mali katikati mwa mji mkuu wa Mali" alfajiri.
Ilisema shambulio hilo lilisababisha "maafa makubwa ya kibinadamu na hasara za mali na uharibifu wa ndege kadhaa za kijeshi."
Makabiliano makali ya moto yalitokea mapema alasiri karibu na kituo cha polisi kinachodhibiti ufikiaji wa uwanja wa ndege wa kiraia, maafisa wa usalama na uwanja wa ndege waliiambia AFP kwa sharti la kutotajwa majina.
'Chini ya udhibiti'
Hapo awali, jeshi la Mali lilisema hali "imedhibitiwa" baada ya kile ilichokiita jaribio la kujipenyeza la "magaidi" katika kituo cha polisi cha kijeshi.
Mamlaka zinazoongozwa na jeshi kwa ujumla hutumia neno "magaidi" kufafanua waasi na wanaojitenga kaskazini mwa nchi.
Kiwango cha shambulio, walengwa, njia zinazotumika na idadi ya wahasiriwa bado haiko wazi, huku kukiwa na udhibiti wa mtiririko wa taarifa chini ya utawala wa junta.
Bamako kwa kawaida huepushwa na aina ya mashambulizi yanayotokea mara kwa mara katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo ya Afrika Magharibi.
Mnamo mwaka wa 2016, watu wenye silaha walishambulia hoteli ya Bamako iliyokuwa na misheni ya zamani ya mafunzo ya Uropa ya jeshi la Mali, na hakuna vifo vilivyoripotiwa kati ya wafanyikazi wa misheni.
"Mapema leo asubuhi, kundi la magaidi lilijaribu kujipenyeza katika shule ya polisi ya kijeshi ya Faladie," jeshi lilisema kwenye mtandao wa kijamii siku ya Jumanne.
"Hali imedhibitiwa," ilitangaza katika matangazo ya redio na televisheni.
Wizara ya usalama ilizungumzia "mashambulizi ya kigaidi" dhidi ya "maeneo nyeti ya mji mkuu", ikiwa ni pamoja na shule ya polisi ya kijeshi.
"Usafishaji unaendelea"
Picha zilizo peperushwa baadaye mchana na kituo cha televisheni cha umma cha Mali zilionyesha karibu wafungwa 20, wakiwa wameketi sakafuni huku mikono ikiwa imefungwa na kufungwa macho.
"Magaidi wamkatwa makali. Msako unaendelea," mkuu wa majeshi Oumar Diarra alisema wakati wa ripoti ya habari ya ORTM lakini hakutaja shambulio kwenye uwanja wa ndege.
Kambi ya mafunzo ya polisi iko karibu na uwanja wa ndege, ambapo kituo cha kijeshi ni jirani na cha kiraia. Wizara ya uchukuzi ilisema katika taarifa kwamba ufikiaji wa uwanja wa ndege "umezuiliwa kwa muda ili kuzuia hatari zozote".
Uwanja wa ndege umefungwa kwa muda
"Uwanja wa ndege wa Bamako umefungwa kwa muda kutokana na matukio," afisa wa uwanja wa ndege alisema, bila kusema utafungwa kwa muda gani.
Shahidi aliithibitishia AFP kwamba eneo hilo lilikuwa limefungwa na kwamba uwanja wa ndege haukuweza kufikiwa kupitia barabara kuu.
Mamlaka haijatangaza rasmi idadi yoyote ya wahasiriwa. Video ambazo hazijathibitishwa zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii zinaonyesha miili chini.
Jeshi linataka utulivu
Operesheni za msako zinaendelea, jeshi lilisema, likitoa wito kwa watu kuwa watulivu na kuepuka eneo hilo.
Milio ya risasi iliyokatizwa na milipuko ilianza mwendo wa saa kumi na moja asubuhi (ndani na GMT), mwandishi wa AFP alisema.
Risasi za hapa na pale bado zilikuwa zikilia asubuhi mapema. Moshi mweusi ulionekana ukitanda kutoka eneo karibu na uwanja wa ndege.
Wamekamwa msikitini
Shahidi alisema yeye na waumini wengine walikuwa wamekwama kwenye msikiti karibu na eneo hilo wakati wa sala ya asubuhi.
Shule ya upili ya Ufaransa, Liberte, ilitangaza kuwa itasalia kufungwa "kutokana na matukio ya nje."
Wafanyikazi katika ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Mali walipokea ujumbe usemao: "Milio ya risasi imesikika katika sehemu za Bamako. Wafanyakazi wote wa Umoja wa Mataifa wanapaswa kuzuia watu kutembea hadi ilani nyingine itakapotolowa."
Mali tangu mwaka 2012 imeharibiwa na makundi tofauti yenye mafungamano na Al-Qaeda na makundi mengine ya waasi, pamoja na majambazi.
Kugeukia Urusi
Ghasia hizo zilisambaa hadi katika nchi jirani za Burkina Faso na Niger.
Mali imetawaliwa na jeshi tangu mapinduzi ya mwaka 2020 na 2021. Chini ya kiongozi wa kijeshi Kanali Assimi Goita, Mali ilivunja muungano wa muda mrefu na washirika wa Ulaya na ukoloni wa zamani wa Ufaransa, na badala yake kugeukia Urusi na kundi lake la mamluki la Wagner kwa ajili ya uungwaji mkono.
Mwaka jana, serikali ya kijeshi pia iliamuru kuondolewa kwa ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kuleta utulivu, MINUSMA, na Januari ilimaliza makubaliano ya amani ya 2015 na makundi yanayotaka kujitenga kaskazini.
Muungano wa Nchi za Sahel
Mali, Burkina Faso na Niger zote zikiwa chini ya uongozi wa kijeshi - waliunda muungano wao wa Sahel mwaka mmoja uliopita na wote waliahidi kujiondoa kutoka jumuiya ya kikanda, ECOWAS.
Hali mbaya ya usalama nchini Mali imechangiwa na mzozo wa kibinadamu na kiuchumi.
Viongozi hao wa kijeshi wameahidi kurejesha udhibiti wa nchi nzima.