kifo cha Lowassa kimesababisha ganzi wa wananchi na jamii za kifugaji za Monduli, mkoani Arusha./ Picha : X- Edward Lowassa

Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Joshua Nassari amekielezea kifo cha Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Ngoyai Lowassa kama pigo kubwa kwa jamii ya wana Monduli.

Kwa mujibu wa Nassari, kifo cha Lowassa kimesababisha ganzi wa wananchi na jamii za kifugaji za Monduli, mkoani Arusha. "Huu ni msiba mkubwa kwa wana monduli, wilaya ni kama imepigwa ganzi," alisema Nassari.

Lowassa anakuwa mbunge wa pili kutoka Monduli kufariki, baada ya Edward Moringe Sokoine, miaka 40 iliyopita.

Hayati Sokoine pia alihudumu kama Waziri Mkuu wa Tanzania kwa mihula miwili, kati ya Februari 13, 1977 na Novemba 7 1980, na kati ya Februari 24, 1983 mpaka Aprili 12, 1984.

Sokoine alijapatia umaarufu kutokana na mapambano yake dhidi ya wahujumu uchumi. Kwa upande wake, mbunge wa Monduli, ambaye pia ni mtoto wa Lowassa, Freddy Lowassa amesema familia yao imepata msiba mkubwa kwa kuondokewa na mwanasiasa huyo mkongwe.

"Nguzo imeanguka, kupoteza mzazi si jambo rahisi lakini tumepokea mapenzi ya Mungu yametimia"

TRT Afrika