Mahakama ya Uswizi inaanza leo kusikiliza kesi ya waziri wa zamani wa Gambia chini ya dikteta aliyepinduliwa Yahya Jammeh kwa mashtaka kadhaa ikiwemo uhalifu dhidi ya ubinadamu.
Hii inatazamiwa kuwa kesi ya kihistoria ambapo mwathiriwa wa ubakaji wa mfululizo atatoa ushahidi baada ya miongo kadhaa ya kusubiri haki.
"Imekuwa kipindi kirefu cha kusubiri, nikingoja kwa hasira, wasiwasi. Lakini nina matumaini makubwa sasa na ninajisikia furaha sana. Ninanusa haki," alisema Madi Ceesay, mlalamikaji mwenye umri wa miaka 67 ambaye anasema alizuiliwa na kuteswa kwa amri ya Sonko.
Waziri huyo wa zamani wa mambo ya ndani Ousman Sonko atakuwa afisa wa ngazi ya juu zaidi kuhukumiwa barani Ulaya chini ya kanuni ya mamlaka ya ulimwengu ambayo inaruhusu uhalifu mkubwa kushtakiwa popote, lilisema kundi la kampeni la Uswizi TRIAL International ambalo liliwasilisha malalamiko dhidi yake.
Walalamikaji tisa wa Gambia watasafiri hadi Uswisi kwa ajili ya kesi iliyopangwa Januari 8-30 katika Mahakama ya Shirikisho ya Jinai huko Bellinzona katika kesi ambayo wanaharakati wa haki za binadamu wanaona kama kuhakikisha uwajibikaji wa kimataifa kwa ukatili mbaya zaidi.
Sonko, 54, anakabiliwa na mashtaka ikiwa ni pamoja na mauaji, ubakaji mara kadhaa, na mateso kati ya 2000-2016 katika kesi ambayo ni ya pili kuwahi kutokea nchini Uswizi kwa uhalifu dhidi ya binadamu. Anakanusha mashtaka.
Wakili wa mshtakiwa Philippe Currat anapanga kuiomba mahakama kuachana na kesi hiyo, kutokana na matatizo ya upelelezi na usikilizwaji.
"Tangu mwanzo nimekuwa nikipigwa butwaa na jinsi kesi hii ilivyoshughulikiwa," aliiambia Reuters, akisema baadhi ya ushahidi katika hati ya mashtaka ulitokana na vikao vya "siri" nchini Gambia na kwamba waliohojiwa hawakufahamishwa kuhusu haki zao.
Currat anasema anaweza kuthibitisha kuwa Sonko alikuwa nje ya nchi wakati mwingi wa tuhuma za ubakaji.
Sonko, alikamatwa mapema 2017 nchini Uswizi, ambapo alikuwa akitafuta hifadhi. Utawala wa ukandamizaji wa miaka 22 wa Jammeh ulimalizika Januari 2017 baada ya kushindwa katika uchaguzi na kulazimika kutoroka.
Sonko anaweza kukabiliwa na kifungo cha maisha ikiwa ndio adhabu ya juu zaidi inayoweza kutolewa na mahakama hiyo.