Kenya leo imefanya hafla ya kuwaaga wauguzi 76 watakaosafiri Uingereza kwa ajili ya ajira.
Wauguzi hao ni kati ya 700 walio omba kupewa nafasi hiyo kufuatia makubaliano kati ya serikali ya Kenya na Uingereza ya kupeleka jumla ya wauguzi 20000, shughuli iliyogawanywa kwa awamu.
Hiini awamu ya pili baada ya kundi la kwanza la wauguzi 19 waliosafiri mwaka 2022 kufatia shughuli ya uteuzi wa ushindani mkali na kisha kupokea mafunzo ya juu maalum ya miezi mitatu kabla ya kusafiri.
Akizungumza katika hafla hiyo katika majengo ya wizara ya Afya jijini Nairobi, waziri wa Afya Susan Nakhumicha, amewasifu wauguzi wa Kenya kama miongoni mwa waliosifika katik autenda kazi wao.
"Wauguzi hawa wanaonyesha roho ya kweli ya sekta yetu ya afya," alisema Waziri Nakhumicha.
"Kujitolea kwao kwa uthabiti na kujitolea kwao bila kuchoka mara nyingi huwa bila kutambuliwa, lakini athari yao haina kifani," waziri alisema.
Waziri Nakhumicha alisema kuwa amepokea taairfa kuwa wauguzi waliotangulia kwenda Uingereza wamepokewa vyema na kuingia katika utoaji huduma bila mashaka yoyote.
Kutafuta ajira bora
Muuguzi mmoja, tumempa jina Lilian kwani hakutaka kutambuliwa ameambia TRT Afrika kuwa, anaunga mkono mpango huu wa kusafirisha wauguzi nje, kwani nyumbani hakuna kazi.
''Hata mimi leo nikipata fursa ya kutoka nitatoka tu,'' ameambia TRT Afrika. ''Hakun ahaja kukaa hapa na kila siku unaona wauguzi wapya wanafuzu vyuo na unajua hakuna ajira.'' Aliongeza.
Lilian ameasema kuwa japo kuna wauguzi wengi wasio kuwana kazi, bado kuna uhaba mkubwa wa wauguzi katik amahospitali za serikali.
''Unajua kila mar aunasikia idadi fulani wamekwenda nje, mara wengine wanastaafu , lakini husikii wakiajiri wapya.'' Amelalamika Lilian. ''Sasa utakuta muuguzi mmoja anahudumia wagonjwa takriban arobaini, ilhali huko nje wenzetu wanashughulikia wagonjwa watatu au wanne kila mmoja.''
Takwimu zinaonesha kuwa idadi kubwa ya wauguzi waliobakia hasa wenye uzoefu wa muda mrefu, wanaamua kutafuta ajira kwa mashirika yasiyo ya kiserikali au hata wakati mwingine kubadili taaluma zao.
Ili kustahiki kazi nchini Uingereza chini ya mpango huu, unahitaji kuwa raia wa Kenya na uwe na diploma au shahada ya kwanza katika uuguzi inayotambuliwa nchini Kenya.
Mhudumu wa afya lazima pia awe amesajiliwa na kupewa leseni na Baraza la Wauguzi la Kenya na awe na cheti cha kibali cha polisi.
Mnamo Julai mwaka huu, Kenya pia ilitangaza kuingia mkataba na Milki ya Kiarabu ya Saudi Arabia, ya kuwapeleka wauguzi na wakunga nchini humo, ili putaka ajira.