Kina mama wa kimaasai wakiwa na bidhaa zao. Picha/TRT Afrika. 

Ronald Sonyo

TRT Afrika, Arusha, Tanzania

Jamii ya Kimaasai ambayo kwa miaka mingi imekuwa ikijulikana kwa ufugaji wa mifugo mbalimbali ikiwemo ng'ombe, mbuzi na hata kondoo hivi sasa inaonekana kubadilisha mfumo wa maisha na kujikita katika shughuli nyengine tofauti na ufugaji.

Kuna sababu kadhaa zinazochangia mabadiliko haya, lakini miongoni mwao ni ile inayotokana na changamoto zilizopo katika ufugaji, hasa kiangazi kikali, uhaba wa malisho, migogoro kati ya wafugaji na wakulima, bila kusahau athari za mabadiliko ya tabia nchi, ikiwemo hali ya ukame, au mvua zilizopitiliza.

Mabadiliko haya yameanza kushuhudiwa katika vijiji vya Esilalei wilayani Karatu na Monduli katika mkoa wa Arusha, kaskazini mwa Tanzania. Baadhi ya wanawake wa jamii ya Kimaasai wameanza shughuli za ufugaji nyuki na uzalishaji wa asali kama sehemu ya kujikimu kimaisha.

Hili ni kundi la takriban wanawake 30 ambao hivi sasa wamekuwa sehemu ya Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Mkoani humo, maarufu MVIWARUSHA. Baada ya kuwezeshwa na Mtandao huo pamoja na kupewa mafunzo ya ufugaji bora wa nyuki, hivi sasa wanaweza kuzalisha na kuliongezea thamani zao hilo kwa lengo la kupanua fursa za masoko.

Hata hivyo, jitihada hizi, hazijalenga wanawake pekee, bali hata wanaume ni wamenufaika.

Miongoni mwao ni Paulo Michael ambae alianza ufugaji nyuki zaidi ya miaka 40 iliyopita. Kwanza alianza kutumia mizinga ya magogo ya miti kabla ya kuhamia katika matumizi ya tairi za gari zilizotumika. Kwa Paulo, baba wa watoto kadhaa ilikuwa ni safari ndefu ya mabadiliko katika sekta ya ufugaji nyuki.

Mizinga yake, ipo umbali wa kilomita tatu kutoka nyumbani kwake.

Mfugaji nyuki akichakata kuzalisha asali. Picha/TRT Afrika. 

Mizinga anayotumia hivi sasa ni ile ya kisasa iliyotengenezwa kwa mtindo wa pembe nne kwa kutumia mbao zilizopakwa rangi nyeupe na kutundikwa kwenye matawi ya miti.

Paulo anaoenekana mwenye kufurahia kazi yake. Wateja wake wakuu ni wafanyabiashara kutoka pande mbalimbali za nchi.

”Nimeirithisha familia yangu ufugaji nyuki na urinaji wa asali kwa sababu tuna uhakika wa kuuza asali, ila vikwazo ni kukosa vifaa maalumu kwa ajili ya sumu ya nyuki,” anasema Paulo, ambae hivi sasa hamu yake kubwa, ni kukamata soko la nje, ikiwemo nchi jirani za Afrika Mashariki.

Paulo kwa msimu mmoja wa mavuno, anaweza kupata debe hadi 25 za asali, ambapo debe moja huwa na lita 20.

Ingawa sio kwa asilimia mia moja, lakini Mtandao wa huo wa MVIWARUSHA umefanikiwa kuingilia kati na kujaribu kutatua baadhi ya changamoto wanazokabiliana nazo wafugaji hao.

Katika hatua ambazo zimechukuliwa ni pamoja na kutoa elimu ya ufugaji bora wa nyuki, uvunaji wa asali pamoja na mazao mengine ya nyuki kama vile masega, nta na kuendelelea.

Baadhi ya mizinga ya nyuki ya kisasa ikiwa imetundikwa katika matawi ya miti. Picha/TRT Afrika. 

Maria Shinini ni katibu wa kikundi cha Emelok Enaisho anakiri ufugaji huo kuleta tija katika jamii. Anasema, kupitia biashara ya asali, wameweza kuwapeleka watoto shule, kujenga nyumba na hata kununua mifugo.

Moja ya mafanikio wanayojivunia nayo ni pamoja na kuunganishwa na Shirika la Chakula Duniani- FAO ambalo wanasema, linawasaidia kupanua wigo na kujiimarisha kibiashara.

Ushirikishwaji wa wanawake

Ushirikishwaji wa wanawake katika harakati za kuzalisha katika jamii, umesaidia kuondokana na mfumo dume uliokuwa umekita mizizi katika jamii hiy ya Kimaasai.

“Kwa sasa tumeondokana na mfumo dume, na tumepata heshima kupitia ufugaji nyuki. Hivi sasa, naweza kujikimu kimaisha na familia yangu. Awali hatukua na fursa za masoko kabisa kwani tulipovuna asali tuliishia kuuzia ndugu na jamaa waliotuzunguka, lakini sasa mambo yamebadilika,” alisema Shinini.

Baadhi ya mizinga ya asali ikiwa shambani. Picha/TRT Afrika. 

Shinini hamu yake ni kuongeza uzalishaji wa asali, lakini hii inahitaji kuwa na mtaji mkubwa zaidi wa kuongeza mizinga ya nyuki ya kisasa, ambapo bei ya kila mzingo, ni takriban dola 50 za kimarekani. Shinini hivi sasa ana jumla ya mizinga 85.

Hata hivyo, safari yao ya ufugaji haikuwa rahisi kama simulizi yake. Kina mama hawa wa Kimaasai wanakiri kupata hasara kwa miaka kadhaa, kutokana na ufugaji na mtindo usio wa kisasa waliokuwa wakiutumia.

Lakini hivi sasa hali imebadilika, na heshima imejengeka.

“Sisi wanawake wa Kimaasai tuliachwa nyuma sana, hatukuwa na uwezo wa kwenda hata sokoni, kusomesha watoto shule na kununua mahitaji na hata kuisaidia jamii. Nililazimika kumuomba pesa mume wangu kila kitu. Lakini sasa kwa zaidi ya miaka minne, tumefarijika mno kwani ninaweza kujikimu,” anasema Phinini.

“Tunafurahi kwa sababu tumeanza kuona mafanikio baada ya kupambana na wanyama wakali wa nyakati za usiku tunapotundika mizinga," anasimulia.

Matumizi ya asali

Zao la asali hutumika kama chakula, dawa na zao la biashara. Aidha asali hutumika kama kiambatio muhimu kama uokaji, viwanda vya vyakula vitamu, vipodozi, vinywaji na viwanda vya dawa.

Tanzania ni nchi ya pili duniani kwa uzalishaji wa asali. Kuna nchi 24 duniani zinazovutiwa na asali ya Tanzania.

Kulingana na sera ya Taifa ya Ufugaji Nyuki ya mwaka 1998 na Mpango wa Taifa wa Ufugaji Nyuki wa Mwaka 2001, Tanzania huzalisha takriban tani 4, 860 za asali kwa mwaka. Hata hivyo, taarifa ya mwaka 2006 ya idara ya misitu na nyuki inaonesha kuwa Tanzania husafirisha nje ya nchi wastani wa tani 500 za asali katika nchi za Ujerumani, Uholanzi, Uingereza, Ubelgiji na mashariki ya mbali.

Kuongeza thamani

Wajasiriamali hao wameanza kuliongezea thamani zao la asali kwa kuchanganya na baadhi ya dawa za tiba za asili na kuuza.

“Tumeelewa thamani ya dawa za asili na tunachanganya na asali na kuuza. Kwa mfano, lita moja yenye dawa tunauza mpaka shilingi elfu 30 za Kitanzania ambazo ni sawa na dola 12 za kimarekani,” anasema.

Changamoto

Lakini mafanikio siku zote hayakosi changamoto. Kutokana na maeneo walipo, ambayo aidha yanapakana au yapo karibu na Hifadhi za Taifa, hivyo wanyama wakubwa kama tembo baadhi ya nyakati huangusha matawi ya miti na kuharibu miundombinu iliyopo. Mbali na hivyo, kuna changamoto pia ya miundombinu ya barabara kutoka vijiji waliopo wafugaji hawa kuelekea sehemu yalipo masoko.

Wastani wa pato la asali nchini Tanzania kwa mwaka, ni sawa na dola 320, na nta kwa mwaka huingiza kiasi cha dola milioni 80. Mapato haya yanaweza kuongezeka kama uzalishaji utaimarishwa.

TRT Afrika