Israel imekanusha vikali mashtaka yaliyoletwa na Afrika Kusini mbele ya mahakama ya ICJ  dhidi yake. Picha ICJ

Ikishutumiwa kufanya mauaji ya halaiki dhidi ya Wapalestina, Israel inatazamiwa kutetea mashambulizi yake dhidi ya Gaza mbele ya Mahakama Kuu ya Umoja wa Mataifa siku ya Ijumaa.

Israeli imekanusha vikali mashtaka yaliyowasilishwa na Afrika Kusini katika mojawapo ya kesi kubwa kuwahi kufikishwa katika mahakama ya kimataifa.

Mawakili wa Afrika Kusini waliiomba mahakama siku ya Alhamisi kuamuru kusitishwa mara moja kwa operesheni za kijeshi za Israel katika Gaza inayozingirwa.

Israel mara nyingi hususia mahakama za kimataifa na uchunguzi wa Umoja wa Mataifa, ikisema kuwa sio za haki na zinapendelea.

Lakini, katika ishara ya jinsi wanavyochukulia kwa uzito kesi hiyo, viongozi wa Israel wamechukua hatua hiyo adimu ya kutuma jopo la wanasheria na kushirikiana na Mahakama ya Kimataifa ya Haki ili kujitetea.

Wanasheria wa Afrika Kusini walisema kuwa vita hivyo ni sehemu ya miongo kadhaa ya ukandamizaji wa Israel dhidi ya Wapalestina.

Wanasheria wa Afrika Kusini waliteta kuwa vita hivyo ni sehemu ya miongo kadhaa ya ukandamizaji wa Israel dhidi ya Wapalestina. Picha ICJ.

"Kiwango cha uharibifu huko Gaza kulengwa kwa nyumba za familia na raia, vita vikiwa ni vita dhidi ya watoto - yote yanaweka wazi kwamba nia ya mauaji ya kimbari inaeleweka na imetekelezwa. Nia iliyoelezwa ni kuharibu maisha ya Wapalestina,” wakili Tembeka Ngcukaitobi alisema katika taarifa yake ya ufunguzi Alhamisi.

"Sifa bainifu" ya kesi hiyo ilikuwa "kurudiwa kwa hotuba ya mauaji ya kimbari katika kila nyanja ya jimbo la Israeli," alisema.

Zaidi ya Wapalestina 23,000 huko Gaza wameuawa wakati wa mashambulizi ya kijeshi, kulingana na Wizara ya Afya katika eneo hilo. "Hakuna kitakachozuia mateso isipokuwa amri kutoka kwa mahakama hii," wakili wa Afrika Kusini Adila Hassim aliwaambia majaji katika chumba kilichojaa watu katika Ikulu ya Amani huko The Hague.

Matokeo ya kesi

Uamuzi juu ya ombi la Afrika Kusini lakutaka mahakama iamauru Israel kusitisha vita pengine itachukua wiki.

Kesi kamili ina uwezekano wa kudumu miaka.

Israel ilianzisha mashambulizi yake makubwa ya anga na ardhini huko Gaza mara tu baada ya shambulio baya la Hamas mnamo Oktoba 7.

Miezi mitatu baadaye, mashambulizi ya Israel yamewafukuza takriban 85% ya wakazi wa Gaza kutoka kwenye makazi yao.

Robo ya wakaazi wa eneo hilo wanakabiliwa na njaa. Na sehemu kubwa ya kaskazini mwa Gaza,imeharibiwa.

Ingawa matokeo ya mahakama yanachukuliwa kuwa ya lazima, haikuwa wazi kama Israel ingetii amri yoyote ya kusitisha mapigano ikiwa uamuzi utakuwa hivyo.

Ikiwa haitafanya hivyo, inaweza kukabiliwa na vikwazo vya Umoja wa Mataifa, ingawa hizo zinaweza kuzuiwa na kura ya turufu ya Marekani.

TRT Afrika