RSF imeshutumiwa kuwatishia wakaazi kwa silaha na ubakaji huku wakiwashutumu kuwasaliti na kushirikiana na jeshi la Taifa./ Picha: Reuters

Wapiganaji wa RSF, kikosi cha dharura cha wapiganaji kilichoingia vitani na Jeshi la taifa Sudan kwa zaidi ya miezi 18 wameshutumiwa kuwatimua wana vijiji katika jimbo la Al jazira Mashariki mwa Sudan.

RSF imeshutumiwa kuwatishia wakaazi kwa silaha na ubakaji huku wakiwashutumu kuwasaliti na kushirikiana na jeshi la Taifa.

"Walisema 'Ulituua, kwa hivyo leo tutakuua na kuwabaka wasichana wako,'" Mmoja wa waathiriwa aliambia Reuters, akijificha chini ya shuka katika mji wa New Halfa, ambapo alifika baada ya kutembea kwa siku kwa miguu na wazee wake.

Salwa Abdallah alikuwa anapata nafuu kutoka kwa upasuaji na kumhudumia mtoto wake wa mwezi mmoja wakati askari wa Kikosi cha Msaada wa Haraka walipoingia nyumbani kwake katika jimbo la El Gezira mashariki mwa Sudan mwishoni mwa mwezi uliopita

Kwa mujibu wa waathiriwa, askari hao wa RSF waliwafukuza wanakijiji wakiwa na viboko na baadaye kuwafyatulia risasi kwenye pikipiki, jambo ambalo majeruhi wengine wawili wa shambulio hilo pia walitaja.

Shirika la habari la Reuters lilizungumza na waathiriwa 13 wa msururu wa uvamizi mkali na wenye vurugu mashariki mwa Gezira katika muda wa wiki mbili zilizopita, ambao uliathiri angalau vijiji na miji 65 kulingana na wanaharakati.

Umoja wa Mataifa unasema takriban watu 135,000 wameyakimbia makazi yao, wengi wao katika majimbo ya Kassala, Gedaref na River Nile, ambayo tayari yamejaa wakimbizi wa ndani zaidi ya milioni 11 kutokana na vita vikali vilivyozuka Aprili 2023.

TRT Afrika na mashirika ya habari