Polisi nchini Kenya wamefukua maiti nane zingine katika ardhi inayo husishwa na kiongozi wa kanisa tatanishi, sasa idadi imefikia 235.
Serikali hata hivyo imesitisha kwa muda shughuli ya kutafuta maiti zaidi ili kuwezesha maafisa husika kufanyia uchunguzi maiti 123 zilizofukuliwa kutoka ardhi inayomilikiwa na askofu Paul Mackenzie.
Askofu huyo anashutumiwa kuwaamrisha wafuasi wake kujinyima kula na kunywa hadi kufa, kwa lengo la kuwakutanisha na Yesu, na kuwa wanaweza kufika mbinguni kabla ya kuisha kwa dunia.
Kufikia sasa watu 89 wameokolewa hai kutoka msitu huo huku watu 31 wakikamatwa kwa mashtaka mbali mbali.
Miongoni mwa wanao zuiliwa na polisi ni askofu Paul Mackenzie, mwanzilishi wa kanisa la Good News International, na mkewe.
Serikali ya Kenya imesema kuwa itawafungulia mashtaka ya ugaidi na mauaji baada ya kumalizika uchunguzi.
Uchunguzi uliofanya kwenye maiti hizo umeonesha kuwa baadhi yao walikufa kutokana na njaa na kunao waliokufa kwa kunyongwa.
Tukio hilo la kushtusha lilisababisha rais wa Kenya William Ruto kuunda tume ya uchunguzi wa vifo hivyo, pamoja na jopo la kufanyia marekebisho kanuni za kusimamia taasisi za kidini.