Serikali ya Ghana imekanusha ripoti kwamba wanamgambo wa Burkina Faso walikuwa wakijijficha katika eneo la kaskazini mwa nchi hiyo na kutumia eneo hilo kama ngome ya vifaa na matibabu ili kuendeleza uasi wao.
Katika taarifa yake siku ya Jumamosi, wizara ya usalama ya Ghana ilisema hakuna "sera ya kutoshambulia au urafiki " au makubaliano ya kimyakimya na makundi ya wapiganaji.
"Wizara inakataa vikali kuonyeshwa kwa Ghana kama 'mstari wa usambazaji' kwa wanamgambo. Juhudi za Ghana za kukabiliana na ugaidi zinapongezwa kwa haki na washirika wake katika mapambano yasiyokoma ya kikanda na kimataifa dhidi ya ugaidi," ilisema taarifa hiyo.
Iliongeza kuwa vikosi vya usalama vya taifa vinashiriki kikamilifu katika juhudi za kukabiliana na ugaidi, hasa katika mpaka wa kaskazini mwa Ghana.
Harakati za kuvuka mpaka
"Serikali ya Ghana, kupitia vyombo vyake vya Usalama wa Taifa na Ujasusi, inaendesha operesheni mfululizo kuzuia uvamizi wowote wa kigaidi au harakati za kuvuka mpaka za wanamgambo na imekuwa ikifanya hivyo kwa miaka mingi kwa mafanikio makubwa," ilisema taarifa hiyo.
Ghana inashiriki mpaka wa kilomita 600 na Burkina Faso, nchi ambayo ni kitovu cha uasi wenye uhusiano na kundi la al Qaeda na kundi la Daesh ambao umeua maelfu na mamilioni ya wengine kuyahama makazi yao katika eneo la Sahel la Afrika Magharibi kusini mwa Sahara.
Waasi wamepata nguvu katika kipindi cha miaka 12 licha ya juhudi za kijeshi zinazoungwa mkono na mataifa ya kigeni kuwarudisha nyuma.
Kufumbia macho
Katika ripoti yake, shirika la habari la Reuters lilitaja vyanzo saba, wakiwemo maafisa wa usalama wa Ghana na wanadiplomasia wa kanda, ambao walisema mamlaka nchini Ghana inaonekana kuwafumbia macho waasi wanaovuka kutoka Burkina Faso ili kuhifadhi chakula, mafuta na vilipuzi, pamoja na kupata wapiganaji waliojeruhiwa kutibiwa hospitalini.
Vyanzo vingi viliomba kutotajwa majina kutokana na unyeti wa suala hilo.
Wizara ya Habari ya Ghana ilikataa kutoa maoni kuhusu habari hiyo.