Viongozi hao wawili wamebadilishana mawazo katika mambo mbalimbali, wakisisitiza umuhimu kati ya Uturuki na Somalia katika utatuzi wa changamoto za pamoja na kuchangia utulivu wa eneo. /Picha: AA

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ameongea kwa njia ya simu na Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamoud, ambapo mazungumzo yao yamegusia ushirikiano kati ya Uturuki na Somalia, kupambana na ugaidi, na masuala ya kikanda na kimataifa.

Katika mazungumzo hayo ya simu siku ya Ijumaa, Rais Erdogan amesema kwamba Uturuki inasimama na Somalia katika mapambano yake dhidi ya ugaidi na kwamba ushirikiano kati ya nchi hizo mbili utaendelea kudumishwa.

Simu hiyo imegusia uhusiano kati ya Uturuki na Somalia, mapambano dhidi ya ugaidi pamoja na masuala ya kikanda na kimataifa.

Rais Erdogan pia amesema kwamba, hali ya wasiwasi iliyopo kati ya Somalia na Ethiopia lazima imalizwe kwa kuzingatia misingi ya kuheshimu mipaka ya Somalia.

Viongozi hao wawili wamebadilishana mawazo katika mambo mbalimbali, wakisisitiza umuhimu kati ya Uturuki na Somalia katika utatuzi wa changamoto za pamoja na kuchangia utulivu wa eneo.

Mkataba wa Makubaliano kati ya Ethiopia na Somaliland

Uturuki siku ya Alhamisi, imeonyesha wasiwasi wake kuhusu Mkataba wa Makubaliano uliotiwa saini kati ya Ethiopia na eneo lililojitenga la Somalia-Somaliland.

Makubaliano hayo yaliyotiwa saini siku ya Jumatatu, yanaipa Ethiopia uwezo wa kutumia eneo la Bahari Nyekundu kupitia bandari ya Berbera iliyopo Somaliland.

Ethiopia ilipoteza bandari yake ya Bahari Nyekundu mwanzoni mwa miaka ya 1990 baada ya vita vya uhuru vya Eritrea, ambavyo vilianza mwaka 1961 mpaka 1991.

Mwaka 1991, Eritrea ilipata uhuru wake kutoka Ethiopia, na kusababisha kuundwa kwa mataifa mawili. Mgawanyiko huo, ulisababisha Ethiopia kupoteza ufikaji wa moja kwa moja katika Bahari Nyekundu na bandari muhimu.

Ethiopia tangu wakati huo, imekuwa nchi bila bahari, na kuathiri uwezo wake wa kufanya biashara kupitia bahari.

TRT World