Denmark inafunga balozi zake nchini Mali na Burkina Faso kama sehemu ya mkakati wake mpya wa Afrika, kwani mapinduzi ya kijeshi "yamepunguza sana wigo shughuli nyingi katika eneo la Sahel," Mamlaka ya nchi hiyo ilisema.
Denmark ilisema itafungua balozi nchini Senegal, Tunisia, na Rwanda na kuimarisha wafanyakazi wa kidiplomasia katika balozi zake nchini Misri, Kenya, Afrika Kusini, Nigeria na Ghana.
Kufuatia kufungwa huko Bamako na Ouagadougou, mwakilishi maalumu atateuliwa katika Maziwa Makuu ya Afrika na eneo la Sahel, imesema taarifa.
Mali na Burkina Faso zimegeukia Urusi na kundi lake la mamluki la Wagner kwa ajili ya kuungwa mkono tangu viongozi wa kijeshi wachukue mamlaka mwaka 2020 na 2022.
Uhusiano wa Mali na nchi za Ulaya umezorota hivi karibuni.
Mapema mwezi huu, uongozi wake wa kijeshi iliamuru ubalozi wa Uswidi kuondoka nchini baada ya Waziri wa Uswidi kukosoa uungaji mkono wa Mali kwa Urusi.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Denmark Lars Lokke Rasmussen alisema upangaji upya wa vipaumbele wa nchi yake barani Afrika unakuja wakati Denmark na Umoja wa Ulaya zikilenga kuwa "mshirika anayependekezwa" wa Afrika.
Amesema huu ni wakati bara likikabiliwa na changamoto ya kuchagua "kujielekeza zaidi Mashariki au Magharibi, " kisiasa.
"Tuna nia ya wazi katika nchi za Kiafrika zinazotuangalia Ulaya wakati zinapanga mustakabali wao," alisema.
Mkakati mpya wa Denmark utazingatia sana kuongeza biashara na mipango ya maji.
Katika miaka ijayo, Denmark inapanga kutoa krone bilioni moja (dola milioni 150) katika usaidizi wa maendeleo kwa mipango mipya ya maji baina ya nchi mbili barani Afrika, na krone milioni 425 mwaka 2025 pekee.