Burundi yatangaza kikosi cha maandalizi ya mechi za kuwania kufuzu Kombe la Dunia mwaka wa 2026

Burundi yatangaza kikosi cha maandalizi ya mechi za kuwania kufuzu Kombe la Dunia mwaka wa 2026

Mshambuliaji Abdou Razak Fiston wa Timu ya Sofapaka ya Kenya ameitishwa tena kwenye kikosi baada ya kutemwa kwa zaidi ya miaka miwili.
Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya Burundi ya soka Intamba Mu Rugamba Étienne Ndayiragije ametangaza kikosi cha maandalizi/ Picha kutoka Akeza Sports 

Ramadhan Kibuga

TRT Afrika, Bujumbura, Burundi

Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya Burundi ya soka Intamba Mu Rugamba Étienne Ndayiragije ametangaza kikosi cha awali cha wachezaji 27 kwa ajili ya kuandaa mechi mbili dhidi ya Gambia na Gabon baadae mwezi huu ili kutafuta nafasi ya kufuzu katika Kombe la Dunia mwaka wa 2026 ambalo litafanyika Marekani, Canada na Mexico.

Kikosi hicho cha Intamba Mu Rugamba, wachezaji wote wanacheza ugenini. Burundi watategemea huduma za nyota wake anayekipiga katika klabu inayoongoza ligi ya Ufaransa ya Nice Yussuf Ndayishimiye lakini pia beki kutoka Vesteras ya Sweden Frédéric Nsabiyumva pamoja na kiungo mshambuliaji wa Simba Saido Ntibazonkiza.

Mshambuliaji Abdou Razak Fiston wa Timu ya Sofapaka ya Kenya ameitishwa tena kwenye kikosi baada ya kutemwa kwa zaidi ya miaka miwili. Anachukua nafasi ya Bonfils Caleb Bimenyimana ambae anauguza jeraha.

Aidha kikosi hicho cha Burundi kimesheheni wachezaji sita kutoka ligi kuu ya Rwanda lakini pia wachezaji 4 kutoka ligi ya Tanzania wakiwemo pia magolkipa Jonathan Nahimana wa Namungo FC na Justin Ndikumana wa Coastal Union.

Na kwa mara ya kwanza nahodha wa Intamba Mu Rugamba Saido Berahino anayechezea Limassol ya Cyprus ameachwa nje ya kikosi sawa na winga Amissi Cedric kutokana na kiwango hafifu.

Burundi itaanza kampeni yake kwa kuipokea Gambia tarehe 16 Novemba kisha kuwaalika Gabon tarehe 19 Novemba. Lakini mechi zote hizo mbili zitachezwa katika Uwanja wa Mkapa Dar es Salaam, Tanzania kutokana na ukosefu wa uwanja Burundi unaokidhi vigezo.

Kocha Mkuu wa Burundi Étienne Ndayiragije amejenga matumaini makubwa kwa kusema, ''Tunahitaji kuweka nguvu za ziada kushinda mechi hizi mbili za mwanzo. Itatupa morali ya kuendeleza vizuri shindano. Gambia ni wazuri saana, wanatumia wachezaji wenye asili ya Senegal. Lakini pia Gabon watakuja na hasira baada ya sisi kuwazuwia kwenda Afcon 2019. Lakini tunaamini tutafanya vizuri ingawa changamoto kubwa tunachezea nje. Ingekuwa bora kama mechi hizi tungezichezea tukiwa nyumbani Burundi.''

Burundi imo katika kundi F pamoja na Côté d'Ivoire, Gabon, Gambia, Kenya na Ushelisheli. Na Kikosi cha Burundi kitaweka kambi yake mjini Dar es Salaam kuanzia tarehe 12 Novemba mwaka huu.

TRT Afrika