Burundi na Uganda, ambazo zinapakana na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, zimeendelea kujiimarisha kiusalama huku machafuko katika eneo la Mashariki mwa DRC yakiendelea.
Hayo yanajiri huku kukiwa na hofu ya kuendelea kwa machafuko katika eneo hilo lenye utajiri mwingi wa madini.
Hivi karibuni, kikundi cha waasi wa M23 wameendelea kudhibiti maeneo kadhaa ikiwemo Goma na Bukavu.
Kikundi hicho kimeendelea kuibua hali ya wasiwasi kwa Burundi, huku maofisa wa kijeshi wa nchi wakisema kuwa imewalazimu kurudisha vikosi vyao nyumbani.
Burundi ilikuwa na zaidi ya wapiganaji 10,000 ambao walikuwa wakitoa msaada kwa Jeshi la DRC dhidi ya waasi wa M23.
"Tumeamua kujipanga kiusalama hasa katika eneo la Kamanyola ili kuwadhibiti wapiganaji wa M23 na wanajeshi wa Rwanda," alisema mmoja ya maafisa waandamizi wa jeshi la Burundi, kwa masharti ya kutotajwa jina.
Hata hivyo, msemaji wa jeshi la Burundi amekana madai ya jeshi la nchi hiyo akisema kuwa majeshi hayo bado yako mstari wa mbele.
Uganda yazidi kujipanga
Wakati huo huo, Uganda imeendelea kusogeza vikosi vyake hadi eneo la Bunia, ambao ni mji mkuu wa jimbo la Ituri.
Tayari, Uganda imepeleka maelfu ya askari katika eneo hilo kupitia mkataba na Kinshasa, ikisisitiza ilikuwa inapambana na wanamgambo.