Bara la Afrika linastahiki heshima zaidi; asema Rais Erdogan

Kwenye taarifa yake maalum aliyoandikia Shirika la Aljazeera, Rais Erdogan anasema kuwa Bara la Afrika linastahiki heshima zaidi kwani nafasi zilizopo za ushirikiano ni nyingi mno. Kiongozi huyo anaongeza kuwa, “Watu wengi duniani wanaihusisha Afrika na umaskini, ukosefu wa usalama na matumaini, dhana ambayo watu wa Uturuki tumeikataa. Tunaamini kuwa Afrika inastahiki heshima zaidi.”

Erdogan ambaye ameandamana na Ujumbe maalum wa Uturuki anazuru Kenya, Uganda na Somalia kwa lengo la kuimarisha uhusiano kati ya Uturuki na mataifa ya Afrika. Kiongozi huyo anasema kuwa Afrika inajivunia kuwa na idadi kubwa ya vijana kinyume na mataifa mengine ambapo idadi kubwa ya watu wapo kwenye umri wa uzeeni. Anaongeza kuwa, “Iwapo dunia itashirikiana, basi wanawake na vijana wa Afrika kwa ujumla wana uwezo wa kufanya mageuzi makubwa ya kiuchumi na maendeleo ndani ya nchi zao.”

Hali kadhalika Rais Erdogan anasema, “Kenya na Uganda kwa mfano zina maeneo makubwa yaliyo na mafuta na vilevile mashamba yana udongo ulio na rutuba ya aina yake na mvua hushuhudiwa mara kwa mara; na sio tu nchi hizi mbili bali Afrika ndivyo ilivyo kwa ujumla.”

Aidha Erdogan alikemea tabia ya baadhi ya mataifa ya nje kujinufaisha na rasilimali kutoka Afrika bila ya kusudi la kweli kuisaidia Afrika katika kusaka suluhu za changamoto zake.

“Iwapo dunia itakoma kujipenda na kuitumia Afrika vibaya basi huenda bara hilo likawa kitovu kikubwa cha maendeleo na mapinduzi ya kiuchumi.” Anasema Rais Erdogan.

Kiongozi huyo alisifia pakubwa hulka ya watu Afrika kuwa wachapa-kazi na wenye fikra za kibiashara pindi tu nafasi inapojitokeza. “Watu wa Afrika wana akili ya biashara jambo ambalo ni muhimu sana kwa vizazi vya kesho na mustakabali wa bara hilo kwa ujumla.”

Akigusia changamoto kubwa zinazoikumba Afrika, Erdogan anasema, “Mataifa mengi kama vile Uganda, Kenya na Somalia yamo vitani dhidi ya magaidi ila wakati uo huo mataifa ya magharibi yanazidi kutengeneza mazingira magumu kwa kujinufaisha huku wakishauri raia wao dhidi ya kuzuru nchi hizo.”

Rais Erdogan anasema kuwa Uturuki itasimama kidete na Afrika katika vita dhidi ya Ugaidi. “Tunafahamu fika changamoto za kiusalama zinazoikumba Kenya, Uganda na Somalia; Uturuki itashirikiana na nchi hizi kwenye vita dhidi ya magaidi.”

Aidha Erdogan anaongeza kuwa Ushirikiano wa Uturuki na Afrika utakuwa ni mfano wa kuigwa duniani. “Pamekuwepo na mengi yanayoendelea baina yetu ikiwemo ushirikiano wa kibiashara na sio tu ziara hizi za kikazi mnazoshuhudia.” Alisisitiza Rais Erdogan huku akigusia maendeleo yaliyoshuhudiwa tangu mwaka 2022 kwa kuwezesha wanafunzi kutoka Afrika kwendfa Uturuki kusoma hasa elimu ya juu.

Akimalizia kwa methali, Erdogan anasema, “Umaskini wa kweli ni ukosefu wa marafiki,” na kuongeza kuwa “Leo na hata milele, Uturuki itakuwa rafiki wa kweli na mshirikia wa karibu wa Afrika.”

TRT Afrika na mashirika ya habari