Mapambo hayo ya jadi hutumiwa na wanawake wa pwani katika kuwapambia waume zao na pia hutumiwa kuzidisha mahaba katika ndoa. Picha/ TRT

Na Fathiya Bayusuf

TRT Afrika, Mombasa, Kenya

Wenyewe husema uzuri wa mwanamke ni kupendeza na kuwa nadhifu wakati wote. Upambe ndio mpango mzima kwa mwanamke mswahili haswa pale anaponogesha muonekano wake kwa kutumia mapambo ya kiasilia kama vile vikuba, vishada na makoja yaliotengenezwa kwa kutumia maua yanayonukia kama mkadi, asumini, viluwa au mawaridi.

“Viluwa, asmini, mlangilangi, mnargisi na mkadi ni maua yenye manukato na yenye umaridadi na haiba yake. Maua haya yanapatikana sehemu za pwani na yanatumika kama pambo hususan kwa wanawake na yana thamani yake. Maua hayo pia ni sehemu ya utamaduni wa waswahili,” akasema Fatma Mohammed ambaye ni mtengezaji vikuba na makoja ya asmini na vilua kutoka mji mkongwe wa Mombasa.

Kutengeza mashada ya asumini mbali na urembo, lakini pia imekuwa ni sehemu ya ajira kwa wanawake.

Mapambo hayo ya jadi hutumiwa na wanawake wa pwani katika kuwapambia waume zao na pia hutumiwa kuzidisha mahaba katika ndoa. Huvaliwa katika sehemu mbali mbali za mwili wa mwanamke kwa mfano kichwani, begani, mkononi na hata kiunoni.

“Kikuba chatengenezwa kwa mkadi, mrehani, vilua, asmini na kikuba kina mawaridi. Mwanamke akivaa kikuba huwa yuwaonekana ni mwanamke wa shani na wa thamani, ni mwanamke anayejua umaridadi na unadhifu. Mwanamke ni vizuri kuvaa kikuba kila siku kuivuta ile haiba ya uke na akaridhisha kwa yule mwenzake ambaye ni mume wake na pia hutela natija nzuri,” akasema Fatma Mohammed.

"Mapambo hayo ya jadi hutumiwa na wanawake wa pwani katika kuwapambia waume zao na pia hutumiwa kuzidisha mahaba katika ndoa. Huvaliwa katika sehemu mbali mbali za mwili wa mwanamke kwa mfano kichwani, begani, mkononi na hata kiunoni."

Fatma Mohammed, mkazi wa Mombasa, Kenya.

Kikuba, kishada au koja hutengenezwa kwa asmini, viluwa, mawaridi au mkadi ambayo hupangiliwa na kuunganishwa kwa uzi kwa kutumia sindano. Mapambo haya kawaida huwekwa ndani ya nyumba ili kuboresha harufu; inaweza kuwa katika eneo la kuishi au chumba cha kulala.

Pia wakati wa sherehe kikuba huwekwa au kishada kwenye kanzu ya wanaume au kwenye bega moja ya mavazi ya wanawake. Wakati wa harusi, ni lazima kwa bibi na bwana harusi kuwa na koja la asumini na viluwa ambalo huwekwa shingoni mwao wakati wa sherehe. Mara nyingi ni rafiki wa familia ambaye huchagua kuleta pambo hilo kama zawadi wakati wa harusi.

“Kishada pia hutengenezwa kwa asmini, vilua na mawaridi na kishada ni tofauti na kikuba. Kishada waeza kukivaa pengine ukiwa uko nyumbani ukishughulika kumpikia mumeo na wanao na pia huleta mvuto na kujenga mahaba zaidi baina ya mume na mke,” akasema Fatma Mohammed.

Siku hizi, fedha pia zinatumika kutengeza mashada ambayo huvaliwa katika shughuli mbalimbali

Kando na asmini na viluwa, sikuhizi pia pesa huchanganywa na maua haya ya kunukia au hutumiwa pekee kutengeneza mitindo tofauti ya vishada na makoja ambayo mara nyingi huvishwa bwana harusi au familia ya maharusi katika sherehe za harusi.

“Ule utengezaji pesa ukimvalisha mtu ni tofauti. Waeza kutengeza zile pesa ukaeka maua ya plastiki lakini koja la pesa hupendeza zaidi likitengezwa kwa mapambo ya asmini na waridi. Mapambo yamekuwa mengi manake sasa hata ukaingia tiktok waona watu wamekuwa wabunifu na wanatumia boxi kutengeneza mtindo wa keki kwa kutumia pesa na kueka na mawaridi, mtu utaona amechukua boxi na kutengeneza mtindo wa nyumba, kanzu au vikapu kwa kutumia pesa na mawaridi yaani inapendeza sana lakini koja la asmini na vilua ndio bora zaidi,” akasema Fatma Mohammed.

Shada lililotengezwa kwa kutumia noti

Utengenezaji wa mapambo haya ya kitamaduni pia umetoa nafasi za ajira kwa wanawake wengi wa Mombasa kama mama Fatma Mohammed huku akijaribu kurithisha ujuzi huu kwa vizazi vijavyo kama njia ya kuhifadhi utamaduni wa mapambo haya ya enzi na enzi. Tima Mohd ni mmoja wa wanaoinukia.

“Nilikuwa namsaidia mama Fatma kutengeza koja, yeye anashikilia upande mmoja na mimi nashika upande wa pili tukitia asmini. Namsaidia kwa sababu wakati mwengine akiwa hayuko basi mimi huwa natengeneza makoja au vikuba. Nimesaidika kupata ujuzi kutoka kwake na pia nashkuru najipatia kipato,” akasema Tima Moh’d, mtengezaji chipukizi wa vikuba na makoja ya asmini na vilua.

Utamaduni huu siku hizi umeonekana kuvutia kwenye sherehe nyengine tofauti kama vile siku ya kuzaliwa au hafla za kisiasa.

Wakati huo huo utamaduni wa mapambo ya vikuba, vishada na makoja ya asmini na viluwa umeonekana kuvutia na kufana hivi sasa mjini Mombasa kutokana na kuzidi kwa matumizi yake kwenye sherehe nyengine tofauti kama vile siku ya kuzaliwa au hafla za kisiasa.

TRT Afrika