Afrika Kusini imesema inatazamia kushirikiana na utawala wa Rais wa Marekani Donald Trump kuhusu sera yake ya mageuzi ya ardhi na masuala yenye maslahi baina ya nchi hizo mbili.
Hii ni baada ya Rais Donald Trump kusema siku ya Jumapili kuwa anapunguza ufadhili kwa Afrika Kusini katika siku zijazo kwa madai ya kunyakua ardhi na unyanyasaji wa "tabaka fulani la watu."
"Afrika Kusini inanyang'anya ardhi na kuwatendea watu wa tabaka fulani vibaya sana. Ni hali mbaya ambayo vyombo vya habari vya mrengo wa kushoto havitaki hata kutaja. Ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu, kwa uchache, unafanyika kwa wote," Rais Trump alisema kwenye mtandao wa kijamii.
Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa mwezi uliopita alitia saini mswada unaoeleza kuwa serikali inaweza, katika hali fulani, kutwaa bila fidia mali ambayo itaamua kurejesha kwa maslahi ya umma.
Msimamo wa Afrika Kusini ni kuwa mswada huo hauruhusu serikali kunyakua mali kiholela na lazima kwanza itafute kufikia makubaliano na mmiliki.
Ikulu ya Afrika Kusini imesema Rais Cyril Ramaphosa atafanya mazungumzo na mwenzake wa Marekani kuhusu suala hili.
" Afrika Kusini inazingatia demokrasia na katiba ambayo imekita mizizi katika utawala wa sheria, haki na usawa," Ofisi ya Rais Ramaphosa imesema katika taarifa.
" Serikali ya Afrika Kusini haijanyakua ardhi yoyote. Sheria ya Unyakuzi iliyopitishwa hivi majuzi si chombo cha kutaifisha, bali ni mchakato wa kisheria ulioidhinishwa kikatiba ambao unahakikisha upatikanaji wa ardhi kwa umma kwa njia ya usawa na haki kama inavyoelekezwa na katiba," imeeleza.
" Afrika Kusini, kama vile Marekani na nchi nyingine, daima imekuwa na sheria za kuhusiana na unyakuzi wa ardhi ambazo zinahusisha mahitaji ya matumizi ya ardhi ya umma na kusimamia haki za wamiliki wa mali," Ofisi hiyo imesema.
Tunatarajia kushirikiana na utawala wa Trump kuhusu sera yetu ya mageuzi ya ardhi na masuala yenye maslahi baina ya nchi mbili.